SERIKALI imesema imeandaa mkakati wa maboresho ya sheria kuwa na sera ya mitandao, itakayodhibiti na kulinda utoaji wa taarifa.
Imesema lengo ni kuimarisha matumizi yenye staha, heshima na utu wa mtu kwa kulinda taarifa zake au taasisi.
Marekebisho ya muswada huo yatawasilishwa bungeni na kujadiliwa, lengo ni kudhibiti wanaokusanya taarifa ikiwemo kampuni za mawasiliano na mtu binafsi kutotoa bila ridhaa yake.
Akizungumza Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Jim Yonazi, amesema mkakati wa maboresho hayo umelenga kuhakikisha marekebisho ya sheria yanazingatia sera bora ya mitandao, itakayodhibiti na kulinda utoaji wa taarifa za mtu au tasisi.
Dk. Yonaz amesema sheria itahakikisha mkusanyaji wa taarifa anatambua wajibu wake kwa kuwa hakuna mwekezaji atakayekuwa tayari kuwekeza katika nchi isiyokuwa na misingi ya udhibiti wa matumizi ya mitandao.
“Sheria hii ambayo muswaada wake utawasilishwa bungeni, italinda taarifa binafsi, yeyote anayekusanya data za mtu ana wajibu wa kuzilinda na utoaji wake uzingatie kanuni na taratibu, sio mtu anakwenda kampuni ya simu kwa kuwa mhudumu ni rafiki yake anamwambia niangalizie huyu nipe taarifa zake,”amesema.
Dk. Yonazi alisisitiza wakati mpango huo ukiendelea kupikwa, ni vyema sheria zilizopo zitumike ipasavyo ili kuimarisha staha, heshima na utu wa mtu kwa kulinda taarifa zake.
Alisema sheria hiyo ikipita bungeni itakuwa bora kwa kuwa serikali inatambua umuhimu wa kulinda taarifa binafsi za mitandao na huduma za mawasiliano nchini.
Katika hatua hiyo alisema ili kuwa na udhibiti wa mitandao ni muhimu kuzingatia taratibu za sheria, haki na kanuni kulingana na nyakati.
“Tunatambua sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 imesisitiza matumizi bora ya mitandao na serikali tunajua mchango wa sekta hiyo katika mafanikio ya kiuchumi, jamii na siasa ndio sababu ya kufanya uwekezaji mkubwa katika Mkongo wa Taifa ambao ujenzi wake ni KM 8319 na umefika mikoa 25 na katika bajeti ya mwaka huu utaongezwa KM 4400,”alisema.
Alisema wanatambua matumizi ya mitandao yameongezeka hatua inayosababisha kuwapo gharama kubwa, hivyo maboresho ya Mkongo wa Taifa na kufungua fursa za uwekezaji katika mikongo ya baharini kutashusha gharama hizo.
Dk. Yonazi alisema mpango wa serikali ni kusimamia upatikanaji wa uhakika wa mitandao na kutoa wito kwa jamii kutumia Kituo cha Utunzaji wa Taarifa (DATA CENTRE), ambacho kinakidhi mahitaji ya vituo vitatu kati ya vinne vikubwa vya taarifa duniani.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema mbali na mipango mikakati iliyopo mradi wa ‘Tanzania Digtal Process’ utaanzishwa hivi karibuni, hivyo ni wajibu wa wananchi kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuongeza ubunifu katika matumizi bora ya TEHAMA.
Mratibu wa Jukwaa la Usimamizi wa Mitandao Tanzania, Nazar Nicholas, alisema wadau watatumia fursa ya mkutano huo kujadili sera ya mitandao, ili kuimarisha ushirikiano na serikali katika kusimamia na kudhibiti upatikanaji wa huduma hiyo kwa bei nafuu, kuimarisha usalama wa taarifa, haki na kanuni.
Na MARIAM MZIWANDA