WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali wafanye biashara kwa uhakika kwa kuwa serikali inataka watimize matananio yao.
“Serikali hii inawatambua na itasimamia matamanio yenu na mtanufaika kwenye ndoto zenu. Mtaji uliowekezwa katika vibanda hivi na Jiji ni shilingi bilioni moja na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akaongeza shilingi milioni 500 ili masoko mengi yajengwe,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja, amekagua masoko ya Mbauda, Kilombero, Machame na kuzungumza na baadhi ya wamachinga wanaofanya biashara katika masoko hayo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wajasiriamali hao baada ya kukagua kila soko, Waziri Mkuu alisema lengo la serikali ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo wakuze mitaji na kumiliki biashara kubwa.
“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan nia yake ni kuwafanya muweze kuwa na maeneo yanayotambulika, kisha mpate kipato rasmi ili nanyi muwe wafanyabiashara wakubwa hapo baadaye. Hapa Arusha wako wafanyabiashara maarufu ambao walianza kwa kusafisha viatu, lakini leo wanamiliki biashara kubwa kubwa,” alisema.
Aliwataka wafanyabiashara hao wafanyebiashara katika maeneo yanayotambulika ili wapatikane kwa urahisi na kupata mikopo ya mitaji kama ambavyo Rais Samia alielekeza.
“Suala la mitaji, Rais Samia alishakutana na wakuu wa mabenki nchini na kuwaomba waweke vigezo ambavyo vitasaidia wajasiriamali wadogo kukopesheka. Ili ukopesheke, ni lazima uwe na anwani, ukiwa na anwani ni rahisi kufuatiliwa unaendeleaje na biashara yako, mtaji wako ni kiasi gani na pia kupima uwezo wako wa kurejesha endapo utapata mkopo.
“Niwasihi ndugu zangu wafanyabiashara, fanyeni biashara zenu kwenye meza zinazojengwa katika masoko. Hiyo meza hapo sokoni ndiyo anwani yako. Uongozi wa soko utajua uko wapi, unauza nini, vina thamani gani. Pia utakudhamini kwa sababu unajulikana unafanyia wapi biashara yako
“Nendeni katika masoko mpate fursa muhimu. Ukikopa, unatakiwa urejeshe ili mwenzio naye apate pia ukimaliza uweze kukopa kiwango cha juu zaidi. Kopeni na kurejesha ili kukuza mitaji yenu, hatimaye mtakuwa wafanyabiashara wakubwa,” alisisitiza.

Mbali na hilo, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa masoko matatu jijini Arusha na kubaini upungufu kadhaa ikiwemo ukosefu wa maji, umeme, uhaba wa vyoo na bugudha za askari mgambo.
Alimwagiza Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda kuhakikisha kero hizo zinaondolewa kwa wafanyabiashara hao.
“Hapa soko la Kilombero nguzo ya umeme iko nje tu, ni kwa nini inachukua mwezi na zaidi kushughulikia ombi la kuweka umeme wakati barua iliandikwa tangu mwezi uliopita? Hiyo shilingi 500 wanayochangishwa, si bora waitumie kununua luku?”alihoji
Mkazi wa Mbauda, Mary Mushi ambaye ni mfanyabiashara ya nyanya katika soko hilo, alimweleza Waziri Mkuu wanachangishwa sh. 500 kununua dizeli ya kuendesha jenereta linalotumika kutoa umeme sokoni hapo. Umeme huo unawashwa hadi saa 3.30 usiku.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alipomtaka Meneja wa TANESCO wa wilaya, Amiri Chambua, aseme ni lini wataweka umeme, Chambua aliahidi kukamilisha kazi hiyo leo.
Pia, alikiri kupokea barua ya maombi tangu mwezi uliopita na kudai walikuwa katika mchakato wa maandalizi.
Kuhusu kadhia ya askari mgambo, Majaliwa, aliwataka watumie weledi na maarifa katika kazi yao ya ulinzi.
“Mtu kama anauza eneo lisiloruhusiwa, askari tumieni miongozo na waeleweshwe na pia zile mali mlizoweka kule Depot warudishieni kwa sababu mitaji ni midogo,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyabiashara hao.
“Nendeni katika masoko mpate fursa muhimu. Ukikopa, unatakiwa urejeshe ili mwenzio naye apate pia ukimaliza uweze kukopa kiwango cha juu zaidi. Kopeni na kurejesha ili kukuza mitaji yenu, hatimaye mtakuwa wafanyabiashara wakubwa” Kassim Majaliwa
Na Mwandishi Wetu, Arusha