WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amesema Julai 10, mwaka huu, anatarajia kwenda nchini Morocco kukutana na wadau mbalimbali ili kuzungumzia nao kuhusu uwezekano wa kuingiza mbolea nchini.
Amesema hadi sasa taifa lina uhitaji wa tani 700,000 za mbolea kutokana na ongezeko kubwa la matumizi yake kwa wakulima.
Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Mwanza, ambapo amesema Wizara ya Kilimo, inawaalika wadau na wawekezaji mbalimbali, kujitokeza ili kuchangamkia fursa ya kuingiza mbolea nchini.
“Wizara ya Kilimo inaalika mtu yoyote kuleta mbolea nchini, cha muhimu aombe kibali kwa kutoka mamlaka yetu ya udhibiti wa mbolea,” amesema Profesa Mkenda.
Waziri huyo amesema kupanda kwa bei ya mbolea kumetokana na ugonjwa wa corona na kwamba hali ikiendelea kuwa ngumu, mkulima atapata changamoto kubwa.
Amesema hivi karibuni, amezungumza na kampuni kadhaa nchini, ili waingize mbolea huku akibainisha kuwa wizara yake imefanikiwa kutatua tatizo la mizigo ya mbolea kukaa muda mrefu bandarini.
Na Johari Shani