SERIKALI imeyafungulia Magazeti manne baada ya kufungiwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, wakati wa kikao chake na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dar es Salaam.
Nape alisema Rais Samia Suluhu Hassan, amemuagiza ayafungulie magazeti yaliyofungiwa na kuwa Rais akisema agizo lake linakuwa ni sheria na sheria inatekelezwa.
“Leo natoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa ambayo ni Mseto, Mawio, Tanzania Daima na Mwanahalisi, hivyo ni vizuri kuondoka kwenye maneno tutende na leseni hizo nazikabidhi leo, kifungo kimetosha, kazi iendelee,”alisema Nape.
Waziri Nape alisema kuwa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwenye tasnia hii ni kuwa karibu na wanahabari.
“Tuzungumze kwa kuwa ninyi ni wadau kwenye maendeleo ya taifa letu, semina hizi zirekodiwe, mawazo ya wanahabari yachukuliwe vizuri ili viongozi tuyachukue na kuyafanyia kazi, tunataka tuboreshe mahusiano yaliyopo katika ya sekta ya habari na serikali, ambapo ameleekeza tupitie sheria, taratibu na kanuni ili ziwe rafiki na kuwezesha utendaji kazi wa wanahabari badala ya kuwa kikwazo kwa wanahabari,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa: “Nakumbuka nikiwa waziri nilipitia Sheria ya Habari na kuisimamia ila mazingira ya wakati ule ya mwaka 2016 na ya sasa ya mwaka 2022 ni tofauti kwa kuwa ni maelekezo ya Rais Samia na tutakubaliana baadhi ya maeneo yaendelee na mengine tutayafanyia kazi kama vile suala la taaluma ya wanahabari tutalisogeza mbele kwa kipindi cha mwaka mmoja ilitulifanyiekazi.”
Alisema anamshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumrudisha tena nyumbani ambapo aliahidi kutekeleza majukumu ipasavyo kwa kuwa habari na teknolojia ya habari ni kama damu na mwili kwa namna sekta hizo zinavyokwenda na zinavyokua hapa duniani.
“Rais amesema anawasalimu ninyi wahariri ambao ni viongozi wenzake na anawaomba muendelee kushirikiana nae kufichua uovu na kuwa jicho lake katika shughuli mbalimbali zinazoendelea nchini,”alisisitiza Waziri Nape.

Katika hatua nyingine, aliiagiza Idara ya Habari – MAELEZO kushirikiana na Jukwa la Wahariri (TEF) ndani ya muda mfupi ili kuwa na kikao na wanahabari kwa malengo ya kujadiliana mapendekezo yaliyopelekwa serikalini ya kuboresha sheria zilizowasilishwa ili zipitiwe upya kifungu kwa kifungu ili kuboresha sekta ya habari nchini.
Pia, aliwashukuru wamiliki wa vyombo vya habari kwa kuwalipa waandishi wa habari waliofariki kwenye ajali ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza pamoja na waandishi waliokuwa wanaidai Kampuni ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwalipa waandishi hao na serikali itaendelea kulinda haki za waandishi wa habari ambapo itatumia sheria, taratibu, kanuni na busara katika kila jambo kwenye uendeshaji wa tasnia ya habari nchini.
Waziri Nape alizielekeza taasisi za serikali zilizokuwa zinasita kutoa matangazo kwa vyombo vya habari, watoe matangazo, walipe madeni kwa kuwa wote wana haki sawa, hakuna haki ya kubaguana.
“Tunajenga nchi moja, nawaomba muitumie vizuri imani ya serikali kama lipo jambo tuongeeni, juzi gazeti liliandika stori kuhusu mabadaliko ya sheria ndogondogo, kutokana na mjadala uliotokea b ungeni, baadhi ya waandishi waliona mwanzo wa mchakato ila hawakuona jambo hilo limeishaje ila mwandishi angefuatilia angetoka na stori iliyo njema, ila Spika angeenda mbali zaidi hali ingekuwa tofauti,”alisema Nape.
Aliongeza kuwa: “Tatizo hatuna muda wa kutafuta ukweli, nawaomba tuaminiane, kama jambo hujalielewa semeni na ni vema wahariri muwalete waandishi wenye uelewa bungeni na wazoefu.
Kwa upande wake, Said Kubenea wa magazeti ya Mseto na Mwanahalisi aliishukuru serikali na Rais Samia kwa hatua hiyo kubwa ya kufungua magazeti hayo.
Balozi Ombeni Sefue ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi Tanzania, alimshukuru Waziri Nape kwa kuchukua jitihada hiyo kwa kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu wa kufanya kazi na serikali na ni wadau muhimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deusdedit Balile, alisema ikitokea ukakutana na mfalme unamsalimia hapo hapo na ukikutana na simba unamkabili hapo hapo, hivyo aliomba serikali ipitie sheria ya vyombo vya habari ili ifanane na za kimataifa.
NA PRISCA ULOMI