SERIKALI imetoa wito kwa washirika wa maendeleo kuiunga mkono katika kufanikisha ufanyikaji wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya kimkakati wa ngazi za juu uliohusisha mawaziri, mabalozi, sekta binafsi na asasi za kiraia, jijini Dar es Salaam.
“Sensa ya Watu na Makazi itaiwezesha serikali kupata takwimu sahihi, kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo, mageuzi ya sekta za kijamii na kuwezesha mamlaka za serikali za mitaa kutekeleza mipango na kugawa rasilimali kulingana na mahitaji,” amesema.
Hata hivyo, amesema wapo baadhi ya washirika wa maendeleo walioanza kuchangia ili kufanikisha sensa hiyo na kuwasisitiza wengine kuendelea kufanya hivyo.
Amesema kuwa mkutano huo umehusisha sekta binafsi na asasi za kiraia kwa kuwa ni wadau muhimu katika maendeleo na kwamba serikali inaweka mazingira wezeshi ili kukua na kutengeneza ajira nchini na kukuza kipato cha wananchi na uchumi.
“Katika mkutano huu serikali imejumuisha asasi za kiraia na sekta binafsi ili zipate taarifa za maendeleo na fursa ya kuona namna ya kushiriki katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya nchi,” alisema.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali, alisema mkutano huo umetoa fursa ya nchi kukutana na washirika wa maendeleo na kuwasilisha mipango iliyopangwa ili kuona namna ya kushiriki.
Akizungumza kwa niaba ya Washirika wa maendeleo Balozi wa Canada nchini, Pamela O’Donnell, alisema kwa muda mrefu wamewekeza mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo endelevu ya nchi na kwamba wapo tayari muda wote.
Alisema washirika wa maendeleo wataendelea kufanya hivyo katika masuala ya elimu, mazingira, afya na utawala bora na wanaamini kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyokusudiwa.
Balozi O’Donnell alipendekeza mambo manne kutiliwa mkazo ikiwemo usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi, demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Alisema mambo hayo ni muhimu kwa amani, maendeleo na jamii endelevu, kuweka mpango mzuri wa kupata nishati, kuhifadhi mazingira na uchumi wa bluu ambavyo visipofanyiwa kazi vina madhara katika maendeleo.
Na Mwandishi Wetu