SERIKALI imepokea chanjo nyingine ya Uviko-19 aina ya Pfizer, dozi 499,590 kutoka Marekani, ikiwa ni mpango wa Covax Facility, huku mikoa 10 ikiongoza kwa watu kupata huduma ya chanjo nchini.
Mikoa inayoongoza ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Dodoma, Arusha, Mwanza, Ruvuma, Mbeya, Morogoro,Mtwara na Kagera.
Imeelezwa chanjo hizo zinatarajiwa kuchanja watu 249,795 na hadi kufikia Novemba 19, mwaka huu, wananchi zaidi ya 1,359,624 wamepatiwa chanjo na kati yao 988,293 sawa na asilimia 1.7 wamemaliza na 371,331 sawa na asilimia 0.6 hawajamaliza dozi yao ya pili ya chanjo aina ya Sinopham.
Akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, alisema katika kupambana na ugonjwa wa Uviko-19, serikali imepokea chanjo dozi 499,590 nyingine aina ya Pfizer kutoka Marekani.
“Serikali inathamini afya za Watanzania, hali inayosababisha kuendelea kuchukua hatua za kuboresha huduma za kinga, hadi sasa tumepokea dozi 1,227,400 za Jensen ambazo zimekinga wananchi 1,227,400 na dozi 2,578,400 za Sinopham zitawakinga 1,289,200,”alisema.
Dk. Gwajima amewahimiza watu ambao hawajachanja kwenda kupata huduma hiyo kwa kuwa ugonjwa wa Uviko-19, upo na unaendelea kusababisha vifo.
Alisema chanjo hiyo Pfizer, itawapa fursa wananchi kuchagua wanayotaka kati ya hiyo, Janseen na Sinopham ambazo zote zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa ni bora na salama.
Alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi na watendaji wa ngazi zote, kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wananchi wanahimizwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma kupata elimu na kuchanjwa.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya afya na miradi mingine ya maendeleo.
Na MARIAM MZIWANDA