JUMLA ya sh. bilioni 8.8 zimetolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa mihadhara wa CDF uliopo Chuo Kishiriki Cha Elimu Mkwawa kilichopo mkoani Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Rasi Utawala wa Chuo hicho, Dk. Fikira Kimbokota, alipokuwa akizungumzia ukamilishaji wa ujenzi wa ukumbi huo na kusisitiza kuwa umesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika kozi zinazohusisha wanafunzi wote wa mwaka husika chuoni hapo.
“Ujenzi wa ukumbi huo ulianza mwaka 2010 na kukamilika Aprili 2020 utakua na uwezo wa kuchukua Wanafunzi 1,209 kwa wakati mmoja na ofisi 14 zenye uwezo wa kuchukua wanataaluma 28,”amesema
Pia amebainisha kuwa zipo kozi ambazo wanafunzi wote wa mwaka husika takribani 1,919 hivyo uwepo wa ukumbi huo utasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki na pia kuwapunguzia wahadhiri kazi kubwa ya kufundisha somo moja kwenye makundi mengi ya wanafunzi.
Ametolea mfano kozi ya Communication Skills inayosomwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 1,919 na kozi ya Ualimu ambazo wanasoma wanafunzi wote kwa mwaka husika wa masomo bila kuwagawa kwa makundi madogomadogo takribani manne na hivi sasa kwa kutumia ukumbi huu wanafunzi watagawanywa kwenye makundi makubwa mawili.
Akizungumzia Sayansi amesema serikali kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imefanikisha ujenzi wa maabara ya Kemia yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 kwa wakati mmoja kwa gharama ya sh. bilioni 2.3 ambapo ukamilikaji wake umepunguza changamoto ya ufinyu wa miundombinu kwa kiasi kikubwa.
Amefafanua kuwa awali walikuwa na changamoto ya ufinyu wa miundombinu kwenye maabara zilizokua zinatumiwa na wanafunzi kufanya tafiti na majaribio ya kisayansi lakini sasa serikali imetuwezesha kupata maabara hii ambayo imepunguza changamoto hiyo.
“Hivi sasa wanafunzi wa Kemia hugawanywa kwenye makundi ya wanafunzi 80 hadi 100 kwa wakati mmoja na hivyo kuwafanya wanafunzi kusoma kwenye mazingira rafiki na kupunguzia kazi Walimu, kwa hakika tunashukuru Serikali kwa kazi kubwa waliyofanya kuboresha Chuo chetu,” amesema.
Amesema ujenzi wa ukumbi huo umesaidia kupunguza matumizi ya wahadhiri wa muda kwani imepunguza mzigo wa kufundisha makundi mengi hivyo wahadhiri kushindwa kupangiwa masomo zaidi ya moja.
Katika hatua nyingine naibu rasi huyo amesema kwa sasa kiasi cha fedha zilizokua zinatumika kuwalipa wahadhiri wa muda kimepungua kutoka sh. milioni 424.7 kwa mwaka wa masomo 2018/19 hadi sh. milioni 103 kwa mwaka wa masomo 2020/21 yote hayo yamefanikishwa na kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi huu.
Na Happiness Mtweve, Iringa