WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa, ametoa maagizo 11, likiwemo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuchukua hatua kwa watendaji na watumishi wa umma wanaoshiriki vitendo viovu vinavyohujumu utekelezaji wa miradi.
Aidha, ametoa wiki mbili kwa TAKUKURU kukamilisha uchunguzi wa ubadhirifu wa sh. milioni 720 uliobainika katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ili hatua zichukuliwe.
Pia, serikali imetoa kibali cha ajira za wahandisi 260 kwa ajili ya kujaza nafasi wazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Maagizo hayo aliyatoa jijini Dodoma, alipokuwa akitoa tathimini kuhusu ziara aliyoifanya mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara na Simiyu, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kusikiliza na kutatua kero za watumishi wa umma kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema katika ziara yake, alifuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati na fedha za kuinua kaya masikini zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mfuko wa TASAF na kubaini kuna wanufaika wanapata fedha licha ya kutokuwa na vigezo.
Kutokana na changamoto hizo, Mchengerwa aliagiza maofisa mipango kusimamia ipasavyo fedha na utekelezaji wa miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa ili ikamilike kwa wakati na kuleta tija iliyokusudiwa na serikali kwa wananchi wake.
Aidha, aliagiza waajiri kuendelea kushughulikia watumishi wenye vigezo na sifa za kupandishwa vyeo kwa kuwatengea bajeti katika mwaka wa fedha ujao na kujiridhisha kama wanastahili.
Mchengerwa aliwaagiza kushughulikia malipo ya stahiki za watumishi, ikiwemo madai ya malimbikizo ya mishahara na kuhakikisha wanaingiza madai hayo kwenye mfumo wa HCMIS kama ilivyoelekezwa katika waraka wa utumizi wa umma Na. 1 wa mwaka 2021.
Pia, kutenga bajeti na kuhakikisha maofisa utumishi wanafanya vikao na watumishi kwa kuwatembelea katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi ili kuondoa malalamiko.
Nyingine ni kutenga bajeti na kuwapelekea mafunzo ya muda mfupi watumishi wa umma na viongozi katika chuo cha utumishi na taasisi za uongozi.
Vilevile, kuwasilisha orodha ya watumishi wenye sifa za kukaimu ili ofisi ikamilishe mchakato wa kujaza nafasi wazi za idara na vitengo, kuimarisha mfumo wa utunzaji siri za serikali kwa kutunza viapo vyao.
Maagizo mengine ni kuongeza uwajibikaji katika eneo la rasilimali watu na fedha katika ukusanyaji mapato kwa kutafuta vyanzo rafiki na kuendelea kutenga bajeti kwa nafasi za msingi zenye upungufu kwa ajili ya kujaza nafasi husika kwa kulingana na uwezo wa kibajeti wa serikali.
Kuhusu TASAF, Waziri Mchengerwa aliagiza watendaji wa halmashauri zote kujiridhisha kwa kufuatilia malalamiko ya kaya ambazo hazikutambuliwa na kuandikishwa kwa kufanya uhakiki.
“Malipo ya kaya mfuate kalenda ili ruzuku zake zitumike vizuri katika mahitaji ya msingi na kukuza uchumi wa kaya. Pia tathimini ifanyike ili kubaini changamoto za malipo kupitia mfumo wa mtandao ili zipatiwe suluhisho,”aliagiza waziri huyo.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema utendaji kazi wa watumishi wanaotekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 watapimwa kutokana na utendaji wao, huku ikitaka utekelezaji ufanyike ndani ya miezi tisa kama ilivyopangwa.
Mchengerwa alisema hayo wakati akizungumzia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa wiki wakati akizindua mpango huo.
Alisema kuanzia sasa watendaji wanaosimamia miradi inayotekelezwa kupitia mpango huo watapimwa uwezo wao kupitia utekekelezaji na kwamba hategemei kuona ubadhirifu unatokea wakati TAKUKURU ipo.
Mchengerwa aliwataka watendaji hao kuandaa mpango utakaowezesha kukamilika katika miezi tisa.
“Watumishi wanaenda kusimamia miradi hii watapimwa utendaji wao kutokana na namna walivyotekeleza agizo la rais kuhusu usimamizi wake kwa kuhakikisha inatekelezwa ndani ya miezi tisa tu na si vinginevyo, ili inufaishe kizazi cha sasa na kijacho.
Alisisitiza wizara hiyo yenye dhamana ya utumishi wa umma na utawala bora itahakikisha maelekezo ya rais yanasimamiwa na utekelezaji wake unafanyika kikamilifu.
AJIRA
Akizungumzia namna serikali ilivyojipanga kukabiliana na changamoto hiyo, waziri huyo alisema tayari kibali cha ajira za wahandisi 260 kimetolewa kwa ajili ya kujaza nafasi zilizo wazi katika mamlaka za Serikali za mitaa.
“Nawapongeza waajiri waliotekeleza kazi ya upandishwaji madaraja kwa watumishi wa umma, ambapo katika ziara yangu nimebaini kuwa waajiri wameitekeleza kazi hii ipasavyo na kupunguza malalamiko kwa watumishi wa umma.
Aidha, alisema alibaini kwamba viongozi walioteuliwa na kuchaguliwa katika maeneo hayo, wanasimamia ipasavyo miradi ya kimakati iliyopo katika maeneo yao ya kiutawala, hivyo kuleta imani kwa wananchi dhidi ya serikali yao.
Mchengerwa alisema kwa upande wa watendaji kata, mitaa na vijiji, tathimini ya mahitaji halisi imeshafanyika na michakato ya kuandaa ajira hizo unaendelea.
Na SELINA MATHEW, DODOMA