ZIKIWA zimebaki siku tano kwa halmashauri zote nchini kukabidhi vyumba vya madarasa vinavyojengwa kwa kutumia fedha za Uviko-19, serikali imesema itazichukulia hatua za kinidhamu zitakazoshindwa kukamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa.
Imesema awali halmashauri zilitakiwa kukabidhi vyumba vya madarasa Desemba 15 kabla ya kuongezewa muda hadi Desemba 31, mwaka huu, hivyo hazitakuwa na sababu za msingi za kuchelewesha ujenzi huo.
Hatua hiyo ilitangazwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, alipozungumza na gazeti hili lililotaka kufahamu hatua zilizofikiwa kuhusu ujenzi huo.
Pia UHURU ilitaka kufahamu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya halmashauri zitakazokwenda kinyume na agizo la serikali la kukabidhi vyumba vya madarasa Desemba 31, mwaka huu.
Dk. Dugange alisema serikali inaamini halmashauri zote zitakamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa.
Alieleza katika kuhakikisha kazi hiyo inakamilika, TAMISEMI iliongeza muda kwa halmashauri zilizopatwa na changamoto ya kukosa vifaa vya ujenzi.
Alibainisha kuwa hawatarajii ucheleweshwaji kutokea na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wote watakaochelewa kukamilisha.
“Hatua stahiki zitachukuliwa kwa kuwa hakutakuwa na sababu ya halmashauri kutokamilisha ndani ya muda. Zitakazochelewa tutazichukulia hatua za kinidhamu,” alisisitiza.
Akizungumzia hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo, Dk. Dugange alisema wakiongozwa na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, wamezunguka katika halmashauri zote nchini, ambapo hadi Desemba 24, mwaka huu, zaidi ya asilimia 90 zilikamilisha ujenzi huo kwa zaidi ya asilimia 98.
Kuhusu madawati, Naibu Waziri huyo alibainisha ukamilishaji ulikuwa ni zaidi ya asilimia 90.
“Kwa mazingira hayo tunaamini ifikapo Desemba 30, mwaka huu, halmashauri zitakuwa zimekamilisha na chache ambazo ni asilimia takriban moja zitakuwa katika hatua za umaliziaji,” alisisitiza.
Aliweka bayana kuwa wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo, baadhi ya halmashauri zilikumbana na changamoto kadhaa zikiwemo kukosa nondo na mabati, kulikosababishwa na ukubwa wa mahitaji nchini.
Pamoja na changamoto hizo, Naibu Waziri huyo, alisema kwa muda uliopangwa kila halmashaurri itakuwa imekamilisha ujenzi wa vyumba hivyo.
Ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ulipangwa kuwa Desemba 15, mwaka huu, lakini serikali iliongeza muda na kuwa Desemba 31, mwaka huu, baada ya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Muda huo uliongezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, baada ya kikao cha tathmini na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe na kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAMISEMI, baada ya kikao hicho cha hivi karibuni ilibainika baadhi ya halmashauri zimepatwa na changamoto katika utekelezaji wa miradi ikiwemo uhaba wa baadhi ya vifaa vya ujenzi.
RC, Ma DED wafunguka
Akizungumza na UHURU, kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, alisema hadi sasa ujenzi wa vyumba vya madarasa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 katika mkoa huo.
Alifafanua kuwa katika Jiji la Arusha, vyumba 16 vya maghorofa vipo hatua za mwisho za utekelezaji na vingine 20 katika Halmashauri ya Arusha vinatarajiwa kukamilishwa kwa mujibu wa maelekezo ya serikali.
Aliwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wanapelekwa shule kwa wakati kwa kuwa, serikali imeshatimiza jukumu lake.
“Watoto waende shule kwa sababu vyumba vimekamilika na viti vyake, tena vimejengwa kwa viwango vya juu na Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, alibainisha kuwa hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 98.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, katika Jiji zima zimebaki shule tatu ambazo kwa sasa mafundi wanamalizia kupaka rangi na anatarajia hadi kufikia Desemba 31, mwaka huu, watakuwa wamekamilisha.
“Ndugu yangu hapa ninapoongea na wewe ndiyo naingia nyumbani kwangu nikitokea katika miradi ya ujenzi wa madarasa, nimetembelea na tupo hatua nzuri,” alisema Shauri alipozungumza naUHURU.
Kuhusu madawati, Shauri alisema sehemu kubwa kazi hiyo imekamilika na kuahidi hadi kufikia siku husika watakuwa wamekamilisha kwa asilimia 100.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Dk. Frederick Sagamiko, alisema katika eneo lake wamekamilisha kwa asilimia 100.
Alisema wanachosubiri ni shule zifunguliwe ili kuanza kupokea wanafunzi bila changamoto kama ilivyozoeleka.
Dk. Sagamiko alisisitiza kwa sababu hakutakuwa na kisingizio cha upungufu wa vyumba vya madarasa, hivyo ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanawapeleka wanafunzi wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza.
Ili kufanikisha hilo, Dk. Sagamiko aliweka bayana wataanza kuhamasisha wazazi kuwapeleka wanafunzi shuleni bila shuruti kupitia watendaji wa mitaa.
FEDHA ZILIVYOTOLEWA
TAMISEMI ilipokea sh.bilioni 535.68 kati ya fedha zote zilizotolewa katika mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 567 (sawa na sh. trilioni 1.3) kutoka Shirika la Fedha Kimataifa (IMF) za kampeni ya
Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 ili kuchangia kufufua uchumi kwa sekta zilizopata athari za kiuchumi kutokana na ugonjwa huo.
Kutokana na fedha hizo za TAMISEMI, serikali ilipanga kujenga vyumba vya madarasa 12,000 vitakavyogharimu sh. bilioni 240 katika shule za sekondari za halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari, mwakani.
Vyumba hivyo vya madarasa vitakapokamilika vitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wote 907,802.
Na JUMA ISSIHAKA