SERIKALI imepewa siku tatu kwa Tume ya Ushindani nchini (FCC), kutoa majibu ya kupanda kwa bei ya vinywaji na kupotea sokoni.
Pia, imeipa tume hiyo siku saba kutoa majibu ya kupanda bei ya vifaa vya ujenzi zikiwemo nondo na saruji.
Maagizo hayo yalitolewa na Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, baada ya kufanya ziara katika ofisi za FCC, Jijini Dar es Salaam.
Dk. Kijaji aliiagiza FCC kupatikana kwa majibu ya haraka ya kupanda kwa bidhaa hizo katika kipindi hiki, hali inayosababisha changamoto kubwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Dk.Kijaji, hali ya upandishaji wa bidhaa imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, bila ya uwepo wa sababu za msingi, huku FCC wakiwa kimya.
“Hii siyo sahihi, tupo kwa ajili ya kulinda walaji. Sasa kama hali inaenda hivi na nanyi mnakaa kimya, sidhani kama mnatekeleza wajibu wenu ipasavyo. Nawataka mfanye uchunguzi makini unaotoa majibu sahihi na kwa haraka, kabla ya wananchi hawapata athari,” alisema.
Alisema watumishi hao wanapaswa kujiuliza iwapo ni sahihi tatizo litokee katika jamii, ndipo watoe majibu au wanatakiwa kutambua changamoto mapema kupitia uchunguzi wao na kuieleza jamii njia sahihi ya kuziepuka.
Pia, aliitaka FCC kuhakikisha wanatembelea katika viwanda mbalimbali vya uzalishaji, ili kujionea hali halisi ya uzalishaji, ikilinganishwa na bei ya bidhaa zinavyouzwa sokoni.
“Mkifanya hivyo mtabaini changamoto ya mabadiliko ya bei ili kuruhusu majadiliano na wazalishaji ya kuweka bei rafiki inayoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi. FCC ni moyo wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, hivyo inaweza kuamua kubadilisha na kuleta maendeleo makubwa.
“Tumeaminiwa na kupewa majukumu haya mazito, hivyo nimeamua tusonge mbele kama kuna mtu hataki hilo na kutaka turudi nyuma sehemu hii siyo yake, atupishe,”alisema.
Mbali na hayo, Waziri huyo alisisitiza kutovumilia uzembe wowote na uvivu huku akisema anatamani kuona mwendo wa mchaka mchaka ili kutimiza malengo.
Aliitaka FCC kufanya uchunguzi na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa bora nchini zinazoendana na uhitaji wa soko la huria la sasa.
“Ni vema mkajitathmini ili kuboresha mipango yenu na kufikia malengo na matarajio ya wananchi. Mkumbuke mmeshikiria uhai wa wananchi kupitia kuwalinda walaji kwa ukaguzi wa bidhaa feki,”alisema.
Waziri huyo aliomba kuongezewa wafanyakazi kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuajiri zaidi ya 15,000.
Waziri huyo alimpongeza Rais Samia kwa kumwamini na kumteua kuwa Waziri na kwamba, atahakikisha anatimiza malengo ya kuaminiwa kwake kwa kushirikiana na FCC.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk. Godwin Otieno, alimshukuru Dk. Kijaji kwa kutambua umuhimu wa FCC na kufanya ziara yake ya kwanza ofisini hapo tangu ateuliwe na Rais Samia.
“Tunakuahidi ushirikiano wa kutosha katika majukumu yako haya. Pia tunatambua kazi kubwa uliyonayo kutokana na ukubwa wa wizara hii na umuhimu wake kwa jamii,hivyo tutakuwa bega kwa bega na wewe,” aliahidi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, alimshukuru Waziri huyo na kuahidi kutekeleza maagizo aliyoyatoa.
SUPERIUS ERNEST NA ZIANA BAKARI