SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imezindua mkakati wa Kitaifa wa Elimu jumuishi wa miaka mitano 2021/22-2025/26 wenye lengo kutoa Elimu jumuishi ambayo itakuwa na mfumo ambao unatoa fursa kwa Wanafunzi wenye mahitaji maalum kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma wakati akizungumza katika uzinduzi wa Mkakati huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa. Eliamani Sedoyeka, kwaniaba ya Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda.
Profesa. sadoyeka amesema Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu bora bila kujali hali aliyo nayo.
“Niwahakikishie kuwa mpango huu utasaidia kuimarisha upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika ngazi zote za elimu,”amesema.
Ametaja lengo lingine ni kuongeza uandikishwaji na ushiriki wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika ngazi zote za elimu.
“Serikali ya Tanzania imesema mkakati wa elimu jumuishi mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026, umelenga katika maeneo mbalimbali ikiwemo kurekebisha sera ya elimu ili iendane na elimu jumuishi katika ngazi zote za elimu,”amesema.
Amesema mkakati huo unalenga kuwajengea uwezo watunga sera, wafanya maamuzi, watekelezaji na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi na namna bora ya kusimamia utekelezaji wake.
Profesa Sadoyeka amesema mkakati huo unalenga katika kuhamasisha utoaji taarifa za utekelezaji wa elimu Jumuishi katika ngazi zote na wadau ili kurahisisha ufanyaji tathimini, kuimarisha njia za ukusanyaji taarifa za elimu jumuishi ili kusaidia ufuatiliaji na kufanya tathimini.
Katibu mkuu huyo amefafanua kuwa Serikali inatambua kuwa, pamoja na kuwa na mfumo wa elimu jumuishi bado kuna wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao hawawezi kuutumia mfumo huo kutokana na kiwango cha changamoto walizonazo.
Amesema ni muhimu kwa Serikali kuwa na mifumo tofauti ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kama shule maalum (Special Schools) na vitengo (Special Unit).
“Nawasii muendelee kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za Serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujifunzaji,”amesema
Katibu mkuu huyo amesema mkakati huo umezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo wanafunzi ambao hawajaingia shule, wakimbizi, wanaotoka jamaii za wafugaji, yatima, wanaotoka familia maskini, wanaotoka maeneo yenye vita na wanafunzi wenye ulemavu.
Amebainisha kuwa mkakati huo pia umezingatia wanafunzi wenye vipawa na vipaji, wanafunzi wenye changamoto za kujifunza, watoto wanaotoka mbali na shule, wanaofanya kazi, watoto wanaolea familia na wanafunzi wenye magonjwa ya kudumu.
Na Happiness Mtweve,Dodoma