WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezindua mpango wa kitaifa wa kuwakopesha wananchi fedha za kufanya urasimishaji wa maeneo yao kwa kipindi cha miaka miwili.
Lukuvi alizindua mpango maalumu wa kukopesha wananchi gharama ya kupanga, kupima na kupewa hati kwa kushirikiana na benki ya NMB, katika Kata ya Igawa, Wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya.
“Mpango huu ni wa nchi nzima, umeanzia hapa Mbarali kwa kuwamilikisha wananchi zaidi ya 52,000, kwa kuwa mazoezi mengi ya urasimishaji yameshindwa kufanikiwa kwa sababu baadhi ya wananchi kushindwakupata fedha kwa mkupuo kugharimia shilingi 150,000 za upimaji na umilikishaji.
Nimeamua kuanzisha mpango huu kwa kushirikiana na NMB ambao watawakopesha fedha za kupanga, kupima na kuandaa hati ambazo benki italipa asilimia 100 kwa mkupuo kisha nyinyi mtalipa utaratibu na kwaawamu kwa muda wa miezi 24 yaani miaka miwili,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, baadhi ya wananchi wamekwamisha kazi ya urasimishaji katika maeneo mengi kwa kuwa wachache ndio wamepata fedha za kugharimia upangaji, upimaji na umilikishaji kwa wakati.
“Sasa NMB leo hapa Mbarali wamekuja kuwakopesha wananchi gharama zote. Na ninataka mchakato kama huu ufanyike nchi nzima na wengine waige kwa kuafuata utaratibu huu; amesema.
Amebainisha kwamba pia asilimia 90 ya wananchi wa Mbarali walikuwa hawakopesheki kwa sababu ya ardhi yao ilikuwa haijapangwa wala kupimwa.
“Lakini kwa mpango huu pia watakuwa na haki ya kukopeshwa na benki yoyote hapa nchini kwa kuwa watakuwa na dhamana inayotambulika kisheria ambayo ni hatimiliki ya ardhi,” amesema
Naye, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kufanya urasimishaji kupitia benki ya NMB ambayo itafanya hilo kwa kutumia matawi yake yote 226 nchi nzima kujipatia mkopo huo na kujiwezesha kiuchumi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Makondo, aliwahakikishia wananchi kwamba wizara hiyo itasimamia kikamilifu mpango huu ambao wananchi watapewa hatimiliki za ardhi za miaka 99 na watamilikishwa kisheria.