KESI ya Uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, imeahirishwa.
Kesi hiyo imeahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya upande wa Jamhuri kuomba ahirisho la kutokana na shahidi wao wa saba kuugua ghafla.
Katika kesi hiyo washitakiwa wengine ni Silvester Nyegu (26), Enock Togolani (41),Watson Mwahomange (27),Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31) wanaokabiliwa na mashtaka matano ya uhujumu uchumi.
Akiomba ahirisho hilo, mbele ya Hakimu Patricia Kisinda katika mahakama hiyo,Wakili wa Serikali Felix Kwetukia, aliomba mahakama hiyo iwape ahirisho la kesi hiyo hadi wiki ijayo kutokana na shahidi wao wa saba Ramadhani Juma ambaye ni mfanyakazi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuugua ghafla.
“Mheshimiwa Hakimu kesi hii imekuja kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri ambapo kwa wiki hii tulipanga kuleta mashahidi wanne, kati yao watatu tayari, sasa huyu shahidi wa wanne ameugua ghafla na hadi asubuhi hii tumewasiliiana naye bado hayuko vizuri, tunaomba ahirisho la kesi hii hadi wiki ijayo,”aliomba Kwetukia.
Alidai nia yao kesi hiyo iendeshwe na imalizike haraka, hivyo aliomba ipangwe mwanzoni mwa wiki ijayo ili mashahidi wa upande wa Jamhuri waendelee kutoa ushahidi.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Utetezi Mosses Mahuna alipinga ombi hilo na kuiomba mahakama hiyo, isikubali ombi la Jamhuri kwa kuwa wana mashahidi 20 na walieleza mbele ya mahakama, hivyo kama shahidi huyo ameugua wangeleta shahidi mwingine.
“Mheshimiwa Hakimu naomba ikikupendeza likatae ombi hili kwa sababu Jamhuri wana mashahidi 20 na walitueleza hapa mahakamani na mpaka sasa wametoa watatu bado 17, hivyo kuugua mmoja kusitukwamishe, walete wengine tuendelee nao, sababu akiendelea kuugua hata mwaka inamaana tutakaa kumsubiri wakati mteja wetu anaendelea kusota ndani,”aliomba.
Hoja hiyo iliungwa na Wakili mwenzake upande wa utetezi Fridolin Gwemelo, ambaye aliiomba mahakama kutokubali ombi la kuahirisha kesi hiyo, kwa sababu upande wa Jamhuri una mashahidi wengi waletwe wengine kesi iendelee.
Pia, Wakili mwenzao upande wa utetezi Edmond Ngemela aliunga mkono hoja za wenzake na kuiomba mahakama hiyo, kutokubali ombi hilo na kudai haki inayocheleweshwa ni hasara kwa pande zote mbili.
Baada ya hoja za mawakili wa utetezi, Hakimu Patricia alitoa nafasi kwa Wakili wa Jamhuri Kwetukia, ambaye aliomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi wiki ijayo kwa madai kupata shahidi ambaye hawajamwandaa ni vigumu na kuna taratibu za kuwaleta mashahidi mahakamani hapo.
Pia, alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imepewa nafasi ya upendeleo maalumu kwa kusikilizwa mfululizo tofauti na kesi nyingine ambazo sheria inasema kila baada ya siku 14 ndio inaendelea, hivyo hakuna haki itakayopotea.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Patricia alitoa uamuzi mdogo kwa kutupilia mbali maombi ya mawakili wa utetezi kwa sababu upande wa Jamhuri uliwasilisha mahakamani uthinitisho wa shahidi wao kuugua.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Patricia aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 27, mwaka huu ambapo mashahidi wa upande wa Jamhuri wataendelea kutoa ushahidi.
Na LILIAN JOEL, Arusha