KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amemtaka Naibu Waziri wa Uvuvi, Abdallah Ulega, kufika wilayani Bukoba na kukutana na wavuvi ili kusikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi.
Amemtaka kuhakikisha anapata nafasi ya kukaa na wavuvi wenyewe na si kupokea ripoti zilizoandaliwa kwa kuwa huenda zisiguse changamoto na mahitaji yao ya msingi.
Shaka aliyasema hayo, alipokuwa akizungumza na wavuvi katika mwaro wa Rushala, Kemondo, ambao walimweleza changamoto mbalimbali ukiwemo usumbufu wanaosababishiwa na maofisa wa mamlaka zinazosimamia mapambano ya uvuvi haramu ambao wamekuwa bughudha kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao bila ya kuzingatia haki.
“Nakuomba Naibu Waziri fika mkoani Kagera ukae na wavuvi, wasikilize shida zao na zitafutiwe ufumbuzi.
Ukifika kutana na wavuvi wenyewe, najua utapewa taarifa zilizoandaliwa hata mimi nimepewa, lakini zipokee kisha kawasikilize wenyewe wanasemaje,” Shaka alimweleza Ulega alipozungumza naye kwa simu akiwa na wavuvi mwaroni hapo.
Shaka alisema uvuvi ni eneo muhimu katika kuzalisha ajira za vijana wengi, hivyo Chama hakiwezi kukubali wanaoshiriki shughuli hiyo wapate changamoto bila ya kutatuliwa.
Kwa mujibu wa Shaka, CCM itaendelea kuwatazama kwa karibu wavuvi ili changamoto zao zitatuliwe na kujengewa mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao.
KILIO CHA WAVUVI
Mmoja wa viongozi wa Jumuiya za wavuvi wilayani Bukoba, Naswiru Kamara, alisema operesheni za kupambana na uvuvi haramu zimekuwa na sura ya uonevu.
Kamara alisema moja ya eneo ambalo utekelezaji wake ni wa kuumiza, ni katika ukamataji wa nyavu zisizokidhi vigezo ambao unawaumiza wavuvi wenye vyombo vikubwa.
Alisema utekelezaji wa operesheni dhidi ya uvuvi haramu, hususan ukamataji nyavu zisizokidhi viwango hazizingatii busara badala yake zimekuwa za kukomoa baadhi ya wavuvi.
Naibu Waziri Ulega alimhakikishia Shaka na wavuvi, kuwa atafika Bukoba na kuzungumza na wavuvi ili kuona namna ya kutatua baadhi ya changamoto zao.
Na MWANDISHI WETU, Bukoba