KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Shaka Hamdu Shaka, amesema katika kipindi cha miaka 45 tangu kuzaliwa kwa CCM, Chama kimekuwa kinara kwa kuchochea mageuzi ya demokrasia Afrika kwa kuendelea kupiga vita siasa chafu zenye mrengo wa ubaguzi.
Amesisitiza CCM itaendelea kuwa Chama sikivu, makini na kujali dhima ya majadiliano kwa njia za kiungwana kuliko kuandamwa na vitisho, kebehi, ubabe au kushurutishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Musoma, Mkoa wa Mara kuhusu mafanikio ya chama hicho kikongwe barani Afrika, ndani ya miaka 45 tangu kilipozaliwa baada ya kuungana vyama vya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), mwaka 1977, alisema kuwa,
CCM iko tayari kupokea maoni, ushauri na maafikiano yanayoheshimu njia za kiungwana na kistaarabu kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Kazi kubwa ya utekelezaji wa sera kwa miaka yote ya utawala wa CCM madarakani ni kuhakikisha umoja wa kitaifa, unadumu na kubaki tukipinga siasa chafu za ukabila, rangi, dini au ukanda badala yake, sera zake zimekuwa zikihimiza umoja na mshikamano, hali ambayo imelifanya Taifa letu kuwa lenye utulivu, upendo na ushirikiano,” alisema.
MAFANIKIO YA CCM MIAKA 45
Akizungumzia mafanikio ambayo CCM inajivunia tangu kuzaliwa kwake, Shaka alisema kwamba, katika kipindi hicho, Chama kimeendelea kuwaongoza Watanzania katika kulinda uhuru wa nchi yao na harakati za kujiletea maendeleo yao.
Alisema mafanikio ya dhahiri, yameonekana kupitia utekelezaji wa sera zake mbalimbali na kujijengea uhalali wa kuongoza nchi katika dunia ya sasa yenye mazingira yanayobadilika kila mara.
“Moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kudumu na kuimarika kwa muungano wetu. Katika kipindi cha miaka 45 iliyopita, muungano wetu umezidi kuimarika kutokana na juhudi za makusudi za chama chetu kuhakikisha muungano wetu unadumu milele.
“Tumefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali ziliyojitokeza katika muungano wetu.
Aliongeza kuwa: “Tumeweza kufanya mambo kadhaa mapya ambayo yamefanya mambo yaende vizuri zaidi. Kitendo cha kuungana kwa TANU na ASP, ndiyo kilichozaa chombo kilichokuwa na nguvu na uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na changamoto za muungano wetu.”
Alibainisha kwa sasa, muungano umekuwa mfano bora wa kuigwa si barani Afrika pekee, isipokuwa duniani kote ambapo Watanzania wameudhihirishia Ulimwengu kuwa, dhamira ya kuungana ni imara na haitetereki.
“Tutaendelea kuimarisha muungano wetu kwa faida ya nchi yetu na watu wetu. Tunafanya hivyo kwa kutambua faida kubwa na nyingi zinazotokana na muungano wetu ambazo kila mmoja wetu anazitambua,” alisema.
UMOJA WA KITAIFA
Shaka alieleza kuwa, mafanikio mengine ambayo chama kinajivunia ni kuimarisha umoja wa kitaifa kama ilivokuwa kwa vyama vya TANU na ASP, sera za CCM zimeendelea kulenga katika kuwaunganisha Watanzania na kujenga taifa moja imara lenye watu wamoja.
Alisema licha ya tofauti za kisiasa, rangi, dini au kabila, kila mmoja anajivunia na kuona faraja kuwa Mtanzania na kuendelea kuimarisha amani, utulivu na mshikamano, mambo ambayo baadhi ya mataifa ya Afrika na duniani ni bidhaa adimu.
“Tumeweza kufanikiwa kubaki kuwa na taifa lenye umoja na utulivu, licha ya nchi yetu kupitia katika kipindi kigumu cha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi na kuingia katika mfumo wa vyama vingi na uchumi wa soko huria. Licha ya umoja wetu hata ukomavu wa kisiasa wa wananchi wetu, pia umeimarika.
“Watanzania ni watu wasioyumba wala kubabaishwa. Ni watu makini, wachambuzi na watambuzi mahiri.
“Haya ni mafanikio makubwa, ni jambo la kujivunia. Lakini ni sifa kubwa kwa chama chetu ambacho ndicho kiliongoza mageuzi hayo nchini.
“CCM itaendelea kuimarisha dhamira yetu ya kudumisha na kuendeleza umoja, amani na utulivu wa taifa letu,” alifafanua.
HUDUMA ZA JAMII
Kwa mujibu wa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, taifa limepiga hatua hatua na kupata mafanikio mbalimbali katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
“Pamoja na kuwa bado nchi yetu ni maskini, hali za watu wetu ni bora zaidi sasa kuliko ilivyokuwa mwaka 1977. Watu wengi wana kipato kikubwa, wanaishi katika nyumba bora zaidi, wanavaa vizuri na wanakula vizuri.
“Utoaji wa huduma za elimu, huduma za afya, maji, barabara, umeme zimeimarika kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Haya yote yanatokana na sera sahihi na mipango mizuri ya Chama Cha Mapinduzi.
MWALIMU WA DEMOKRASIA
Kuhusu demokrasia, alieleza kuwa, CCM imekuwa mwalimu wa Demokrasia nchini, mataifa jirani na kimeweza kusimamia na kuongoza nchi kufanya uchaguzi, wananchi kutumia mamlaka na haki zao za kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na Utulivu.
Aidha, alisema CCM ndani ya miaka 45, imefanikiwa kusimamia muundo wa sera, mikakati na aina ya siasa inayohitajika katika nyakati za sasa, jambo lililosaidia kulinda na kusimamia usalama wa taifa na watu wake ili kudumisha amani, umoja na kujivunia uhuru wake.
Alisema kazi kubwa ya utekelezaji wa sera kwa miaka yote ya utawala wa CCM madarakani ni kuhakikisha umoja wa kitaifa unadumu na kubaki kupinga siasa chafu za ukabila, rangi, dini au ukanda badala yake, sera zake zimekuwa zikihimiza umoja na mshikamano hali ambayo imelifanya taifa kuwa lenye utulivu, upendo na ushirikiano.
“Katika nyakati zote, kila mwananchi amekuwa mlinzi wa Taifa lake, askari wa mstari wa mbele anayehakikisha hatokei adui akayejivisha koti la kuwa kibaraka au wakala, badala yake mapambano yameelekezwa dhidi ya maadui ujinga, umasikini na maradhi,” alisisitiza.
USHIRIKIANO KISIASA
Shaka alisema kwa miaka yote 45, CCM imekuwa mstari wa mbele kuendeleza na kudumisha ujirani mwema ili kujenga haiba ya maendeleo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kudumisha uhusiano mwema, kuendeleza ushirikiano na vyama vingine rafiki na vya kidugu duniani ikiwemo kanda ya Afrika Mashariki.
Alieleza CCM, imeendeleza mahusiano hayo ili kuhakikisha ujirani mwema unadumu, unaendelezwa kwa kuwaletea manufaa wananchi wa Tanzania na mataifa mengine.
Vilevile, alisema CCM katika kipindi cha miaka 45, imekuwa chachu ya kuanzishwa kwa kamati ya nchi tano zilizo mstari wa mbele kusini mwa Afrika, kipindi ambacho mataifa kadhaa yalikuwa bado hayajapata uhuru.
Kwa kushirikiana na vyama vingine vya ukombozi, CCM kimekuwa na mchango kwa mataifa hayo kushamirisha juhudi za ukombozi hadi mataifa hayo yalipopata uhuru na kujitawala yenyewe.
“Dhana ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ni kutanuka kwa wigo wa demokrasia shirikishi, ushindani wa sera kwa sera, ujenzi wa hoja kwa nguvu ya hoja. Kwa kipindi chote cha miaka 45 CCM kimeendelea kuwa Chama sikivu na makini kwa nyakati zote.
“Kinapenda na kujali dhima ya majadiliano kwa njia za kiungwana kuliko kuandamwa na vitisho, kebehi, ubabe au kushuritishwa. CCM kipo tayari wakati wote kupokea maoni, ushauri na rai hatimaye kufikia kwa maafikiano yanayoheshimu njia za kiungwana na kistaarabu kwa maslahi mapana ya taifa letu,” Shaka alieleza.
Alitoa wito kwa Watanzania kuendeleza umoja, mshikamno wa taifa na kuendelea kuvisihi na kuviomba vyama vyote vya siasa nchini kuendeleze umoja wa kitaifa, kuthamini na kukuza ustawi wa demokrasia iliopo nchini.
Alisema yapo mataifa mengi duniani hivi sasa yanatamani yafanane na Tanzania lakini kwa bahati mbaya haiwezekani baada ya baadhi ya wanasiasa wao kuvuruga amani yao.
Shaka alisema mafanikio hayo yamekuwa msukumo mkubwa wa ujenzi wa imani kwa wananchi wa Tanzania na imani hiyo itaendelea kulindwa na kuheshimiwa kwa utiifu.
“Kwa namna ya pekee Chama Cha Mapinduzi kinamshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyojipambanua tangu alipochukua hatamu ya uongozi wa kuliongoza taifa kwani ameonyesha uwezo, juhudi na jinsi alivyodhamiria kukabiliana dhidi ya changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa katika kusukuma maendeleo endelevu ya nchi yetu,” Shaka alieleza.
NA MUSSA YUSUPH, MUSOMA