KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii, kupeleka mara moja tochi maalumu za kusaidia kufukuza tembo kwa vikundi vilivyoundwa kukabiliana na wanyama hao wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu.
Amesema ulinzi wa wananchi dhidi ya wanyama wakali na waharibifu, ni jukumu muhimu ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na kwamba, hatua ya wananchi kujitolea kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuzuia wanyama hao, zinapaswa kuungwa mkono.
Shaka ameyasema hayo kwa nyakati tofauti akiwa wilayani Meatu, alipokuwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama katika mashina kama sehemu ya ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo mkoani humo.
“Nitazungumza na Wizara ya Maliasili na Utalii leo (jana), walete tochi zinaohitajika. Nimeambiwa kuna vikundi vya wananchi vimeundwa na vinahitaji tochi hizo kwa ajili ya kusaidia kufukuza tembo wanaoingia katika makazi ya watu, wizara ilete haraka tochi hizo,” amesema.
Amesema maelekezo ya CCM kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Ibara ya 69 vifungu vidogo vya (b) na (c), Chama kinaitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, iweke mikakati thabiti ya kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori kupitia vifaa maalumu vya kuwafukuza au kuwazuia wasifike maeneo ya makazi.
Pia, ameeleza kuwa, Ilani inaielekeza wizara hiyo, kuwajengea uwezo wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi kupitia vikundi ili wawe na uwezo wa kuwafukuza wanyamapori wanapovamia maeneo yao bila madhara.
“Hatuwezi kutukuza uhifadhi unaowaumiza wananchi wetu na kuwapa umaskini huku kukiwa hakuna hatua stahiki zinazochukuliwa. “Hali hii ikiachwa hivi, wananchi watachoka, wataanza kuwadhuru wanyamapori tulionao wakiwemo tembo wanaovamia katika mashamba na makazi ya wananchi na kuleta madhara,” amesema.
Shaka amesema kuwa, CCM inahimiza uhifadhi endelevu unaojali maendeleo na ustawi wa maisha ya wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi za wanyamapori, hivyo wizara ya maliasili, ichukue hatua za haraka kuwanusuru wananchi dhidi ya usumbufu wa wanyamapori katika maeneo yote nchi nzima yanayopakana na hifadhi, ili kero ya uvamizi wa wanyama idhibitiwe.
Kauli ya Shaka imetokana na kilio cha wananchi katika mashina matatu ya CCM aliyoyatembelea kukagua uhai wa Chama ambayo ni Shina Namba 4, Tawi la Ng’hoboko, Shina Namba 4 Tawi la Imalaseko na Shina Namba 4, Tawi la Kimali ambako kote walilalamika tembo kuingia katika makazi ya wananchi na kuharibu mashamba.
Mbali na hilo, Shaka amewahakikishia wanachama wa CCM na wananchi wa wilaya hiyo kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kutekeleza ahadi zote zilizoahidiwa kupitia Ilani hiyo ya CCM, hatua kwa hatua.
Ameeleza kuwa, utekelezaji huo unaendelea kwa kasi katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu, vituo vya afya na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Awali, katika risala ya wazee wa wilaya hiyo walipokutana na Shaka, iliyosomwa na Mzee Emmanuel Masanga, walimpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayofanya ikiwamo kuweka historia ya kuwawezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuanza masomo kwa pamoja.
Mzee Emmanuel alisema wazee wa wilaya hiyo, wanaiona kwa macho kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia na kwamba, wataendelea kumuunga mkono huku wakihamasisha vijana kuchapa kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.
KUHUSU UCHAGUZI WA CCM
Akizungumza aliposhiriki Mkutano wa Balozi wa Shina Namba 4 Tawi la Ng’hoboko, Shaka aliwataka wana CCM kujiandaa na uchaguzi wa ndani ya Chama utakaoanza mapema mwaka huu.
Shaka amesema; “CCM inataka kuona viongozi wenye sifa wanapewa nafasi ya kuongoza ili kukisaidia Chama kiendelee kuwa cha wananchi na kuharakisha maendeleo ya taifa.”
Shaka aliwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi, kuomba nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama na jumuiya zake ili kuunda safu imara ya uongozi wa CCM utakaowaletea maendeleo wananchi.
Na MWANDISHI WETU, Meatu