KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama kinataka kuona madiwani wake nchi nzima wanafanya kazi ya kuwatumikia wananchi ikiwemo kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo.
Pia, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma kwa kujenga machinjio ya Kisasa na kufanikisha ajira kwa vijana zaidi ya 31, akisema hilo ndilo ambalo Chama linataka kuona katika halmashauri mbalimbali nchini.
Akizungumza katika Kata ya Mbetele, Manispaa ya Songea, Shaka, amesema kila diwani anapaswa kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo katika eneo lake na kupokea kero za wananchi.
Amesema CCM inataka kila diwani afanye kazi kuendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia wananchi hususan wanyonge.
“Wananchi wa Songea niwaombe endeleeni kuiamini CCM, muaminini Rais wetu ambaye anafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya taifa letu ili kuendelea kuleta huduma kwa kila Kijiji, mtaa na kata nchini nzima,” alisema.
Aidha, Shaka aliwasihi madiwani kusikiliza kero za wananchi kwa wakati na siyo kusubiri viongozi wa kitaifa wanapofika katika maeneo yao, ndipo waanze kufanya vikao, “sasa nawaagiza madiwani kufanya kazi kwa kuendana na kasi ya Rais wetu.”
“Niwahakikishie wananchi wangu wa Songea na Tanzania kwa ujumla, serikali yenu ipo makini katika kutatua kero zenu, Rais Samia Samia anakuja na kasi ya juu katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma iliyo bora zaidi,” alisema.
Aidha, Shaka aliwaomba wananchi kuendelea kujitolea katika kazi za maendeleo ndani ya maeneo yao ili miradi ya maendeleo ikuwe kwa kasi na kuendana na juhudi za Rais Samia.
AIPONGEZA MANISPAA YA SONGEA
Akizungumza katika machinjio ya halmashauri hiyo, Shaka alisema serikali imetoa zaidi ya sh. bilion 10 kutekeleza mradi huo. “Hapa nimeamini kweli Ilani ya Uchaguzi ya CCM Manispaa ya Songea imefanya vizuri, niwaombe mwendelee hivyo hivyo katika kusimamia Ilani ipasavyo.”
Aliongeza:”Nimefurahishwa na mradi wa machinjio ya Manispaa ya Songea, nimeona usimamizi mzuri na ushirikiano mzuri katika ujenzi wa mradi huu na nimeona jinsi mlivyokuwa wamoja na wazalendo wa nchi yenu.”
Kwa mujibu wa shaka, CCM inaendelea kusimamia Ilani yake ya uchaguzi katika sekta ya ufugaji wa kisasa ili kuhakikisha unakuwa kwa kasi na kujenga miradi mingi za ya machinjio.
Mbunge wa Songea Mjini, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Damas Ndumbaro, alimpongeza Shaka kwa kuona namna Manispaa ya Songea inavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo, kuhakikisha mradi huo unatimia.
Na SOPHIA NYALUSI, Songea