KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amezitaka Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kukutana na kufanya mapitio kuhusu misitu ya hifadhi iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
Shaka ametaka uwepo wa misitu katika wilaya hiyo, uwe neema na kuleta manufaa kwa wananchi.
Shaka aliyasema hayo, wilayani Tanganyika, alipozungumza katika vikao mbalimbali kikiwemo cha wazee wa wilaya hiyo, alipokuwa katika ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, iliyofika mkoani humo kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na uimara wa Chama mashinani.
“Maelekezo ya Chama wizara hizi zikutane, zijadili kwa pamoja suala hili na kuja na mwafaka wa pamoja kuhusu misitu iliyopo Tanganyika.
“Lengo letu ni kuona tunaitunza kwa ajili ya ustawi wa mazingira yetu, kuchochea utalii lakini kubwa zaidi, ni lazima wananchi wanufaike nayo,” alisema.
Shaka alitoa maelekezo hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa kulinda na kuihifadhi misitu ya Nkamba, Tongwe Mashariki na Tongwe Magharibi, ambazo zimekuwa zikiwabana na kusababisha katika baadhi ya maeneo kuwa na eneo dogo la kufanyia shughuli zao za kiuchumi kikiwemo kilimo.
Shaka aliwataka wadau hao kukutana na kujadili vifungu mbalimbali vya kisheria, vinavyohusika katika uhifadhi misitu na kutwaa maeneo kwa ajili ya uhifadhi na kuhakikisha sheria zinazingatiwa.
Awali, akizungumza katika Kijiji cha Kasekese, katika Jimbo la Mpanda Vijijini, wilayani Tanganyika, Mbunge wa jimbo hilo, Moshi Kakoso, alisema Juni 25, mwaka huu, serikali kupitia tangazo Namba 460 imeanzisha eneo jipya la pori la akiba linaloitwa Luganzo-Tongwe, katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
Alisema tangazo hilo jipya limechukua eneo lote la Msitu wa Tongwe Mashariki wenye hekta 167,832 sawa na ekari 414,720.
Mbunge huyo alisema pia tangazo hilo limeingilia eneo la Luhafwe, lililotengwa na halmashauri ya wilaya hiyo, kwa ajili ya uwekezaji wa kiuchumi.
MAAGIZO MENGINE YA SHAKA
Akiwa katika eneo la ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Karema wilayani humo, Shaka aliipongeza serikali kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kifungu cha 59 ibara ndogo (b) na (v), inayosisitiza kuhusu ujenzi wa miundombinu hususan ya bandari.
Alisema ujenzi wa bandari hiyo utafungua fursa kwa uchumi wa mkoa wa Katavi, Rukwa, Kigoma na maeneo mengine yanayozunguka eneo hilo na taifa kwa ujumla.
Shaka alieleza kuwa, ujenzi wa bandari hiyo, ambao sasa umefika zaidi ya asilimia 60, unaonyesha dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika na kuongeza vichocheo vya ukuaji wa uchumi.
Na MWANDISHI WETU