KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, ametoa maelekezo kwa taasisi za umma zenye miradi mikubwa, kuwa na bajeti maalumu itakayosaidia kuhudumia miradi hiyo kwa maslahi ya wananchi.
Ametoa maelekezo hayo alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo Mjini Babati, ambapo alitembelea maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo, likiwemo lililosimikwa mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni.
Alisema ni muhimu katika kulinda miradi mikubwa kuweka utaratibu wa taasisi zote kuwa na fedha ambazo zitatumika kutatua changamoto zinapojitokeza ili huduma ziendelee kutolewa kwa wananchi.
“Tujenge utamaduni wa kuwa na bajeti maalumu itakayotumika kuhudumia miradi yenye thamani kubwa ili kuilinda,”alisema Shaka akiwa katika hospitali hiyo baada ya kupata taarifa za uwepo wa changamoto mbalimbali hasa ya uchakavu wa jengo na kukatika kwa umeme kulikosababisha baadhi ya vifaa vya mtambo huo kuungua.
Kutokana na changamoto hiyo, Shaka alizitaka wizara husika kujenga majengo yenye hadhi yake, kuwa na mkakati wa kuilinda isiharibike.
Shaka alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuitekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambayo imezungumza vizuri kuhusu uboreshwaji wa sekta ya afya.
”Unaposoma Ilani ya uchaguzi kifungu G ibara ya 83 inaeleza kuimarisha hospitali 28 nchini kuwa za rufaa na hospitali hii ni miongoni mwao,”alisema Shaka.
Awali, Kaimu Mganga Mfawidhi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara Dk.Yesige Mutajwaa, alimpongeza Rais Samia kutoa fedha hatua iliyoleta ufanisi kwa kusimika mtambo wa hewa tiba ya oksijeni.
“Uendashaji wa mtambo huo unafanywa na wataalamu wa vifaa tiba na majukumu yao ni kuhakikisha mtambo unafanya kazi kwa ufanisi, kutoa ripoti kwa timu ya uendeshaji wa hospitali kuhusu uzalishaji wa hewa hiyo na utendaji kazi wa mtambo
“Usimikaji wa mtambo ulianza Februari 7 mwaka huu, japo usimikaji wa mtambo huo wa kujazia mitungi hewa haukukamilika kutokana na kuungua kwa conractor ya dryer. Umekamilika Machi 12, 2021 na umeanza kutumika Aprili 8, 2021.
”Unaposoma Ilani ya uchaguzi kifungu G ibara ya 83 inaeleza kuimarisha hospitali 28 nchini kuwa za rufaa na hospitali hii ni miongoni mwao”. Shaka Hamdu Shaka.
Na MWANDISHI WETU, Babati