WANACHAMA 445 kutoka vyama vya CUF na ACT Wazalendo kisiwani Pemba, wamevihama vyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwemo aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Konde kwa tiketi ya CUF, Salama Hamis Omary.
Pia Chama kimepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuwaunganisha Wazanzibari kuendeleza umoja wa kitaifa na mikakati madhubuti ya kujenga uchumi imara.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alipozumgumza na viongozi wa ngazi mbalimbali za Chama katika Kijiji cha Chimba, Jimbo la Tumbe Wilaya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo Wanachama 45 walikabidhiwa kadi kwa niaba ya wenzao wote.
Shaka amesema kazi zote za utekelezaji wa kisera lazima ziende sanjari kati ya Chama na serikali bila kutegeana, kwa kuwa kufanikiwa kwa mipango na malengo ya utekelezaji wa kisera ni jukumu la kila mmoja.
“Chama kinapongeza juhudi za dhati zinazochukuliwa na SMZ chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi, tangu aingie madarakani amekuwa kiungo anayehubiri na kuhimiza dhima ya kuendeleza umoja wa kitaifa na mshikamano,” amesema.
Amesema nchi au taifa lolote duniani halitapata mafanikio ya kupigiwa mfano na kusonga mbele na kufikia shabaha za kisera, ikiwa kuna baadhi ya watu wanabeza mshikamano kudhoofika kwa maelewano au kukosekana utulivu na amani.
“Kazi ya kiongozi bora ni lazima awe na utashi au uwezo wa kuwaunganisha wananachi wake, msingi wa maendeleo unahitaji kudumisha umoja wa kitaifa, utulivu na kuweka malengo ya muda mfupi na mrefu na kuandaa mazingira bora na endelevu,” ameeleza Shaka.
Amesema kazi za kisiasa ni lazima zitokane na nguvu ya umoja watu wawe tayari kufanyakazi kwa ushirikiano, maelewano na kuvumiliana bila kubaguana au kuanzisha makundi ya utengano na hasama.
“Kadri taifa linavyopiga hatua za kuleta maendeleo lazima zijitokeze changamoto na vizingiti. Kazi ya viongozi ni kuhakikisha wanaendeleza umoja, kuzikabili na kuzipatia majibu changamoto husika bila kugawanyika au kutegeana,” amesema.
Katibu Mwenezi amesema Rais Dk. Mwinyi anashuhudiwa anavyojituma, anavyochukua hatua kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kwa lengo kuongeza wigo wa ajira kwa vijana na kuhimiza utendaji wa pamoja, nidhamu ya kazi na uwajibikaji.
Na Mwandishi Wetu, Pemba