KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama kitasimamia ahadi yake ya kuheshimu, kulinda demokrasia na haki za binadamu ili kudumisha umoja, amani na ustawi wa taifa.
Aidha, amempongeza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa kuonyesha uungwana kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na kuahidi ushirikiano wa dhati.
Shaka alisema hayo jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja tangu Mbowe aachiwe huru kutoka gerezani baada ya DPP kuondoa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
“Ibara ya 118 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuheshimu na kulinda misingi ya demokrasia na haki za binadamu kwa ajili ya kudumisha umoja, amani na ustawi wa taifa kwa kuzingatia katiba ya nchi,” alisema.
Alisema siasa safi ni pamoja na kutanguliza maslahi ya nchi na kushirikiana katika mambo ya msingi yanayogusa maslahi ya taifa.
“Siasa safi inahusisha uzalendo, utu, heshima na kuweka mbele maslahi ya Taifa kuliko chochote. Rais Samia ni kielelezo katika hili na ameendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuijenga Tanzania moja yenye ustawi kwa wananchi wote. Tumpe ushirikiano,” alisema.
Kwa mujibu wa Shaka, lengo la CCM katika kipindi hiki ni kuhakikisha kuwa, wananchi wanaendelea kupata haki kwa mtu mmoja mmoja na makundi mbalimbali na kuongeza: “Tunampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza maelekezo haya ya Ilani kikamilifu, hakika kazi inaendelea vyema.”
MBOWE
Mbali na hilo, Shaka alipongeza kitendo cha uungwana kilichoonyeshwa na Mbowe kwa kumshukuru Rais Samia.
“Namshkuru Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kuonesha uungwana, kwa sababu amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali na amemuahidi kumpa ushirikiano kwa ustawi wa Tanzania. Hiyo ndio siasa safi na hiyo ndio Tanzania tunayojivunia,” alisema.
Shaka aliwahakikishia wananchi kwamba, Chama kitaendelea kusimamia serikali izidi kuimarisha uhuru wa kutoa maoni.
“Chama Cha Mapinduzi kinawahakikishia Watanzania kuwa, kitaendelea kuisimamia serikali izidi kuimarisha uhuru wa maoni, misingi ya haki na demokrasia ili kujenga taifa lenye upendo, umoja, amani na mshikamano wakati wote,” alisema.
IKULU
Awali, Mbowe alikutana na Rais Samia na kufanya nae mazungumzo Ikulu, Dares Salaam, zikiwa ni saa chache baada ya kuachiwa huru.
Katika mazungumzo hayo, Mbowe alimshukuru Rais Samia kwa uongozi wake na kusimamia haki, umoja na mshikamano.
Na MWANDISHI WETU