WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema katika mwongozo, vigezo na sifa za kunufaika na mikopo ya elimu ya juu, hakuna kigezo mahususi cha shule aliyosoma mwombaji na mnufaika.
Hayo yameelezwa bungeni, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Omary Kipanga, wakati akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni (CCM) Ussi Salum Pondeza.
Katika swali lake mbunge alihoji, serikali haioni kuwa umefika wakati wa wanafunzi wote kunufaika kwa asilimia 100 bila kujali shule walizosoma?.
Aidha, alihoji serikali inawasaidiaje wazazi waliostaafu ambao wameshindwa kuchangia gharama za elimu ya juu?.
Akijibu swali hilo, Kipanga alisema mikopo inayotolewa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ambayo inaelekeza walengwa wa mikopo hiyo ni wahitaji.
Alieleza uhitaji wa mwanafunzi hupimwa kwa kuchambua taarifa zilizowasilishwa wakati wa maombi ya mkopo, zikiwemo gharama za masomo ya sekondari au stashahada.
Alifafanua kuwa, uchambuzi huo hutumia king’amua uwezo ambacho hubaini kiwango cha uhitaji cha mwombaji mmoja ukilinganisha na wengine.
Aidha, alisema uhitaji wa mnufaika unatumika kuamua kiasi anachopangiwa kulingana na gharama ya shahada aliyodahiliwa.
“Baada ya uchambuzi linganishi, waombaji hupangiwa mikopo kulingana na uhitaji wao. Katika mwongozo, vigezo, sifa za kunufaika na mikopo ya elimu ya juu, hakuna kigezo mahususi cha shule aliyosoma mwombaji na mnufaika,”alisema.
Kuhusu waombaji wa mikopo ambao wazazi wao wamestaafu katika utumishi, alisema serikali inaamini utaratibu wa sasa wa kutambua na kuwapangia mikopo wahitaji wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama za elimu ya juu kwa watoto wao unajitosheleza.
“Hata hivyo, serikali ipo tayari kuendelea kupokea maoni ya namna ya kuboresha zaidi utaratibu huu,” alifafanua.
Na SELINA MATHEW, Dodoma