JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu sita kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu ambao wamekuwa wakitumia mbinu ya kuwafunga kamba walinzi wakati wakiwa wanatekeleza uhalifu huo.
Pia, limefanikiwa kuzuia jaribio la uporaji wa gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 374 DKR lilokuwa linataka kuibwa na majambazi wanne eneo la Kibamba Wilaya ya Ubungo ambapo katika kupambana nao askari walifanikiwa kumjeruhi mmoja ambaye alikimbizwa hosptali na baadae alipoteza maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema tukio hilo lilitokea Novemba 14 mwaka huu saa tatu asubuhi ambapo kabla ya majambazi hao hawajatekeleza adhima yao askari walifika eneo la tukio na majambazi hao walipobaini uwepo wa askari walianza kurusha risasi.
“Tukio hili lilitokea Novemba 14 majira ya saa tatu asubuhi ambapo majambazi wanaokadiliwa kuwa ni wa nne wakiwa na silaha huku wakitumia gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T311 DLQ walijaribu kuiba gari aina ya Toyota IST.
“Kabla ya kutekeleza adhima yao kikosi kazi cha kuzuia na kupambana na uhalifu sugu kilifika eneo la tukio,walipobaini kuna askari walianza kuwarushia risasi na Polisi wakajihami na kufanikiwa kumjeruhi mmoja ambaye alikimbizwa hosptali na baadae alipoteza maisha” alisema
Aidha akifafanunua kuhusu watuhumiwa sita wa tuhuma za unyangaji, Kamanda Muliro, amesema watu hao walikamatwa na dola za Kimarekani 2,000, Laptop moja saa za mkononi tisa, simu nne na gari aina ya Gala, lenye namba za usajili T274 CBH vitu ambavyo vimepolwa eneo la Upanga Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amebainisha kuwa wamefanikiwa kukamata gari aina ya Toyota Ractis lenye namba za usajili T 775 DUM lililokuwa limeibwa na kutolewa taarifa kituo cha polisi Kigamboni Dar es Salaam huku watuhumiwa wawili wakishililiwa kwa kuhusika na wizi huo.
Aidha, Kamanda Muliro amesema watuhumiwa wote watafikishwa Mahakamani baada ya taratibu zote za kisheria kukamilika.
Na IRENE MWASOMOLA