SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imejipanga kufanikisha dhana ya uchumi wa buluu, kwa kuhamasisha matumizi endelevu ya bahari ili kupata ajira za kudumu.
Akizungumza katika mkutano wa wadau kuhusu mapitio ya rasimu ya uchumi wa buluu, Chake Chake, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahor Massoud, alisema uwekezaji katika uchumi wa bahari, umefikiwa kwa kutambua uwezo na mpango wa maliasili na rasilimali za pwani na baharini, zinazozunguka visiwa vya Zanzibar.
“Tayari mpango wa kununua vyombo umekamilika na tunaendelea kujipanga zaidi kuwapatia wavuvi vyombo vya kisasa na mitaji, kwa ajili ya kuimarisha hali zao,” alisema.
Aidha, alisema serikali ya awamu ya nane, inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, imejikita katika kuboresha masoko ya samaki yaliyopo na kujenga mapya, ambapo suala hilo litakwenda sawa na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata minofu na kusindika samaki kwa ajili ya soko la ndani na nje ya Zanzibar.
Alitaja uvuvi mdogo na ule wa bahari kuu, ufugaji wa samaki, uchimbaji wa mafuta na gesi, utalii wa fukwe na michezo ya baharini ni maeneo ya kipaumbele katika kufanikisha dhana hiyo.
Akiwasilisha mada ya dhana ya uchumi wa buluu, Ofisa Uratibu, Shaaban Hassan Ramadhan, alisema ni matumizi endelevu ya rasilimali za baharini, mito na maziwa kwa ajili ya ukuzaji uchumi, maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira.
Mjumbe wa Timu ya Maandalizi ya Sera ya Uchumi wa Buluu, Kitwana Makame Kitwana, alisema serikali itahakikisha inaimarisha usafiri wa bandarini na uendeshaji wa viwanda.
Akiwasilisha mada ya sera ya uchumi wa buluu, Kitwana alisema miongoni mwa changamoto zinazopaswa kutatuliwa ni uvuvi usio endelevu unaotokana na mazoea hatarishi na kupokea bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Kitwana alisema Zanzibar ina rasilimali ya bahari, ndiyo maana ikaundwa Wizara ya Uchumi wa Buluu ili kusudi kukuza uchumi kupitia bahari, hivyo hakuna budi kuitumia vyema rasilimali hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dk. Salim Mohamed Hamza, aliwataka viongozi hao kuwa na sauti ya pamoja katika kuwaelezea wananchi sera ya uchumi wa buluu ili waifahamu na kuifanyia kazi.
Akichangia mada katika mkutano huo, Ofisa Mdhamini Tume ya Mipango Pemba, Khamis Issa Mohamed, alisema wananchi wa Zanzibar hawajaelewa dhana ya uchumi wa buluu, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuwaelimisha.
Na ALI NGOME ALI, PEMBA