SPIKA wa Bunge Job Ndugai ameiagiza Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti Stanslaus Nyongo, kukaa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kujadiliana sababu za kuvuja kwa mitihani ya utabibu na nini kifanyike.
Hayo ameyasema bungeni baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majabu na kabla ya kuanza kwa mjadala wa mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2022/23.
“Nimesikia mitihani imevuja, hivyo kamati ikae na Waziri mjadiliane mjue sababu za kuvuja kwake na kabla ya Ijumaa mje na ‘Way forward’ nini kifanyike kuhusu hili.” amesema Spika Ndugai.
Hivi karibuni,Serikali ilitangaza kurudiwa kwa mitihani ya utabibu ngazi ya tano ndani ya wiki sita kuanzia Novemba mosi mwaka huu huku ikieleza mtaalamu wa afya aliyejipa sifa kwa njia ya udanganyifu ni hatari kwa afya ya wananchi.
Aidha, ilisema uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watu/vyuo/taasisi zingine zilizojihusihsa na udanganyifu huo ili kuwachukulia hatua walioshiriki kutekeleza hilo.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichwale aliyasema hayowakati akitoa ufafanuzi kuhusu kuvuja kwa mitihani hiyo hali iliyopeleka kufutwa.
“Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(NACTE) limeagiza kurudiwa kwa mitihani hiyo upya ndani ya wiki sita na itafanyika sambamba na mitihani ya marudio kwa program zingine za afya nchi nzima,”.
Wizara ya Afya inawaelekeza wakuu wa vyuo vyote vya afya kuwapa taarifa wanafunzi ili wajiandae kwa ajili ya mitihani hiyo,”alisema.
Aidha, alisema wizara imesikitishwa na tukio hilo na itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha uchunguzi na kuwachukulia hatua walioshiriki kufanya udanganyifu na kuwataka wanafunzi wa vyuo kuzingatia masomo na kutojihusisha na vitendo hivyo.
Awali alifafanua baada ya kutokea taarifa za kuvuja kwa mitihani hiyo, iliundwa kamati ya uchunguzi ambayo ilibaini kuwa mitihani hiyo ilisambazwa kupitia mitandao ya kijamii ambayo ni Telegram na WhatsApp na kuonekana kwenye baadhi ya namba za simu za wanafunzi zilizofanyiwa uchunguzi.
Alibainisha wanafunzi hao walipohojiwa walikiri kupata mitihani hiyo kupitia makundi ya mitandao ya kijamii yaliyoanzishwa na wanafunzi hao kwa ajili ya kujadiliana.
“Kamati ya uchunguzi imewasilisha taarifa ambayo imethibitisha kuwepo kwa udanganyifu kwenye baadhi ya vyuo vilivyochunguzwa kupitia namba za simu za wanafunzi.
Uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watu/vyuo/taasisi zingine zilizojihusihsa na udanganyifu huo na taarifa hiyo iliwasilishwa kwenye Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi(NACTE) Oktoba 24, 2021 kwa ajili ya maamuzi kwani ndio chombo cha kisheria chenye mamlaka na vyuo vya elimu ya kati nchini,”alisema.
Alibainisha katika kikao cha 78 cha NACTE kilichokaa Novemba Mosi, 2021 taarifa hiyo ilijadiliwa, kupitia sheria ya Baraza sura 129 na kanuni za mitihani, kifungu 33 (1) (iii), 2004 (GN.75) limefuta matokeo ya mitihani ya nadharia kwa masomo yote ya utabibu ngazi ya tano.
Mitihani ya muhula wa pili kwa mwaka wa masomo 2020/21 ilifanyika kitaifa kuanzia Agosti 16, 2021 hadi Septemba 2021 ambapo siku ya mwisho ya ufanyikaji wa mitihani ya nadharia wizara ilipokea taarifa za kuwepo kwa viashiria vya kuvuja kwa mitihani hiyo.
NA SELINA MATHEW, DODOMA