BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Dar es Salaam, limesema swala ya Eid El Hajj itafanyika Julai 21, mwaka huu kitaifa, katika Msikiti wa Mtoro.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambapo swala hiyo itafuatiwa na Baraza la Eid litakalofanyika katika msikiti huo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Sheikh wa Mkoa Alhad Mussa Salum, amewataka waislamu kujitokeza kwa wingi kushiriki swala hiyo inayoambatana na ibada ya kuchinja.
“Tupo katika miezi ya hija na waislasmu baada ya ukamilifu wa hija huwa wana swala ya Eid El Hajj. Hii ndiyo Eid kubwa kuliko Eid El Fitri.
“Kitaifa itaswaliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Hivyo ni heshima kubwa kwa waislamu wa mkoa huu,”amesema Sheikh Alhad.
Sheikh Alhad amesema Julai 21, ambayo itakuwa Jumatano itakuwa ni mapumziko ya kitaifa hivyo kuhimiza waislamu kushiriki kikamilifu.
“Swala hii itaswaliwa Saa 1:30 asubuhi. Baada ya hapo itafuatiwa na Baraza la Eid yaani tutaunganisha na vyote vitafanyika katika Msikiti wa Mtoro,” amebainisha Sheikh Alhad.
Na Ashura Assed | 📸 Christopher Lissa