MFUKO wa Misitu Tanzania (TaFF), umesema tangu kuanzishwa kwake umewezesha miradi 673 ya ufugaji nyuki na upandaji miti Tanzania Bara, ambayo imekuwa chachu ya uhifadhi wa mazingira na rasilimali misitu nchini.
Umesema uwezeshaji wa miradi hiyo kwa Watanzania umeigharimu TaFF takriban sh. bilioni 30 kuanzia Julai mwaka 2011 hadi Julai mwaka huu.
Akizungumza na Uhuru, Katibu Tawala wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Dk. Tuli Msuya, alisema miradi hiyo iliyogharamiwa inahusisha ruzuku ndogo, ya kati, kubwa na ruzuku maalumu.
Katibu Tawala huyo alisema miradi ya ruzuku ndogo ni ile isiyozidi sh. milioni 10, ruzuku ya kati isiyozidi sh. milioni 20, ruzuku kubwa haizidi sh. milioni 50 na ruzuku maalumu ambayo ni zaidi ya sh.milioni 50 na kuendelea kwa kadri bodi ya wadhamini itakavyoona inafaa.
Dk. Tuli alisema mfuko huo umekuwa ukiwawezesha Watanzania ruzuku ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ufugaji nyuki na upandaji miti.
“Tunatoa ruzuku sio mkopo kwa maana tunampa mtu fedha akatekeleze shughuli iliyokusudiwa na hatakiwi kurudisha, tunafanya hivi ili kuongeza uhifadhi,” alisema.
Aliwataja walengwa wa ruzuku hiyo ni watu binafsi ambao wanapaswa kuomba ruzuku ndogo ya hadi sh. milioni tano na vikundi vya kijamii ambavyo vitatakiwa kuomba hadi sh. milioni 10.
Dk. Tuli aliwataja walengwa wengine kuwa ni Mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yatatakiwa kuomba miradi ya kuwezesha taasisi na mashirika ya kijamii, asasi za kiraia, taasisi za serikali na za utafiti na mafunzo.
Kuhusu vigezo vya upataji wa ruzuku hiyo, alisema kwa watu binafsi wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaokubalika, ambao mara nyingi wanapaswa kuwa watumishi wa serikali katika eneo husika linalotekelezwa mradi.
Alisema wanafanya hivyo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinatumika kutekeleza miradi iliyokusudiwa.
Dk. Tuli alitaja vigezo vya vikundi kuwa na usajili kutoka katika mamlaka husika, NGO’s na asasi za kiraia lazima zisajiliwe na kuhakikiwa, mashirika ya dini yawe yamesajiliwa na taasisi za serikali huwa zinatambulika kwamba zimesajiliwa.
Katibu Tawala huyo alisema vigezo vya jumla ni kwamba, ruzuku hizo hutolewa kwa mdau ambaye tayari alishaanza kufanya shughuli husika na shabaha ni kuboresha mradi wake.
“Kama ni upandaji miti angalau uwe umeshaanza kupanda sasa unataka tukuwezeshe uongeze au uboreshe mradi,” alisema.
Alisema kigezo kingine ni kuandika mpango wa uendelevu wa mradi hata ruzuku itakapokwisha, kuonyesha uwezo wa kutekeleza mradi husika ikiwemo namna ya ushirikishaji wa wataalamu na lazima eneo la mradi liwe Tanzania Bara.
Katibu Tawala huyo, alisema wanafanya hivyo kwa sababu Wizara ya Maliasili na Utalii si ya Muungano, hivyo utekelezaji wa miradi lazima ufanyika Tanzanioa Bara.
Alitaja kigezo kwa waombaji wa ruzuku ya kati na kubwa wanapaswa kuonyesha kwamba watachangia asilimia 20 ya kiasi wanachoomba katika mfuko na hiyo sio lazima iwe fedha bali hata kufanya baadhi ya shughuli.
Dk. Tuli alisema moja ya mafanikio ya mfuko huo ni kuifikia mikoa yote Tanzania Bara, kuhamasisha ufugaji nyuki na kuifanya TaFF kuanzishwa viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki.
Alisema hilo limefanywa zaidi katika mikoa iliyoonekana kuwa na uhitaji mkubwa wa masoko kutokana na uzalishaji wake.
Katibu Tawala alitaja maeneo vilivyopo viwanda hivyo ni Kibondo (Kigoma), Sikonge (Tabora) na Bukombe (Geita), ambavyo vyote vimeanzishwa ili kuitangaza asali ya Tanzania.