MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salum Rashid Hamduni, amewaagiza wasaidizi wake ngazi za wilaya na mikoa ukiwemo Dar es Salaam, kuendelea kuchunguza miradi iliyokataliwa na Mwenge wa Uhuru.
Mwenge huo ulishindwa kuzindua baadhi ya miradi ya maendeleo katika baadhi ya wilaya za mkoani wa Dar es Salaam, baada ya kubaini dosari za majengo kujengwa chini ya kiwango na kutoendana na thamani halisi ya fedha.
Hamduni alisema hayo alipozungumza na UHURU kuhusu kushindwa kuzinduliwa kwa baadhi ya miradi jijini Dar es Salaam na hatua walizoanza kuzichukua kuhusiana na suala hilo.
“Kweli tulipata maagizo kutoka kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu, Sahili Geraruma, aliyetutaka tufuatilie miradi yote ambayo Mwenge umeshindwa kuizindua kwa dosari zilizojitokeza, hivyo tunaendelea kuyatekeleza kwa uchunguzi,” alisema.
Aliwasisitiza wasaidizi wake waliopo ngazi za wilaya na mikoa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya uchunguzi kwa wakati katika miradi yote iliyokataliwa na Mwenge ili kazi iendelee.
Kwa mujibu wa Hamduni, kazi yao inaishia ngazi ya uchunguzi, hivyo wanaendelea na utaratibu huo na utakapokamilika watawasilisha mrejesho kwa ngazi husika ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na kanuni.
“Uchunguzi ni jambo linalochukua hatua mbalimbali, hivyo linafanywa kwa umakini ili kubaini dosari zilizojitokeza katika miradi hiyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Hamduni alisema wanaendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
“Kamati yangu yangu iko Dar es Salaam inaendelea na kazi ya uchunguzi, itakapokamilika tutawajulisha,” alisema.
Naye, Mkuu wa TAKUKURU, Mkoa wa Temeke, Hole Makungu, alibainisha wameshaanza kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na kiongozi wa mbio za mwenge kwa miradi iliyokuwa na dosari.
Aliwataka viongozi wengine wanaosimamia miradi ya maendeleo wilayani humo kuisimamia vema ili kuepuka vitendo vya ubadhilifu vitakavyowafikisha katika vyombo vya kisheria.
Alitaja miradi waliyokabidhiwa kwa uchunguzi ni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari ya Karibuni wenye thamani ya sh. milioni 135 na jengo la kujifungulia na upasuaji Zahanati ya Kilakala lenye thamani ya sh. milioni 250.
Miradi mingine inayochunguzwa na Mwenge huo ni ile iliyopo Wilaya za Ubungo na Kinondoni.
REHEMA MAIGALA na SUPERIUS ERENEST