TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Wilaya ya Tarime, imewaonya watakaothubutu ‘kudokoa’ zaidi ya sh. bilioni nne zilizotolewa na serikali kwa Halmshauri za Tarime Mjini na Tarime Vijijini, kujenga madarasa zaidi ya 120 ya Shule za Msingi na Sekondari.
Akizungumza na Waandishi wa habari, ofisini kwake, Kamanda wa Takukuru, Wilaya ya Tarime, Protas Sambagi, alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha hizo kwa ajili ya kugharamia ujenzi huo, si watu kuzikwapua.
Alisema sh. bilioni 2.3, zitatumika kujenga madarasa 116 ya halmashauri ya Tarime Vijijini ambapo kila darasa, litajengwa kwa sh. milioni 20, sh. milioni 300 zitatumika katika uchimbaji kisima kirefu cha maji katika Mji wa Sirari.
Aidha, alieleza kuwa, sh. milioni 250 zitatumika katika ujenzi wa Kituo cha Afya Bumera yakiwemo majengo matatu ya maabara, wagonjwa wa nje na jengo la kuchomea taka.
Kamanda huyo wa TAKUKURU, alisema katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, wamepewa sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari mpya ya Nkende baada ya wananchi wa kata hiyo kutoa eneo la ujenzi na sh. milioni 560 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 28.
Alisema sh. milioni 80, zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule shikizi madarasa manne ambapo kila darasa, litagharimu sh. milioni 20, sh. milioni 300 zimetolewa kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na sh. milioni 200, zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje.
“Takukuru inafuatilia matumizi ya fedha hizo za miradi zilizotolewa na Rais Samia kwa ajili ya maendeleo kwa wananchi wa Tarime Mjini na Vijijini.
“Tunatoa onyo kwa wale wote wenye nia mbaya ya kufikiria kuhujumu fedha hizo za miradi ya maendeleo kuwa hawatabaki salama,” alisisitiza.
Aliwaomba watumishi wa halmashauri, viongozi wa vijiji, kata na wananchi kuwa makini kuwafichua wale watakaojihusisha kwa vitendo vya ubadhirifu.
Naye Mwenyekiti wa Halmasahuri ya Mji Tarime, Daniel Komote, aliishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo za maendeleo, aliahidi kusimamia vyema matumizi yake.
Na SAMSON CHACHA, TARIME