SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeingia makubaliano ya ununuzi wa magari na mitambo yenye thamani ya zaidi ya bilioni 15 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Hifadhi za Taifa.
Makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania (REGROW) unaoendeshwa chini ya mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia. Hifadhi zitakazonufaika katika makubaliano hayo ni Ruaha, Mikumi,Udzungwa na Nyerere
Utiaji saini wa makubaliano hayo umefanyika makao makuu ya TANAPA ambapo Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema, alisaini mikataba na makampuni ya Al Mansour Auto EA Tanzania Ltd na Hughes Agricultural Tanzania Ltd, yaliyoshinda zabuni ya kusambaza magari na mitambo hiyo.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo, Kamishna Mwakilema, amezitaka kampuni hizo kukamilisha taratibu zote kwa haraka, kwa mujibu wa mikataba yao, ili kuwezesha upatikanaji wa mitambo na magari hayo kwa wakati.
Mwakilema ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi za kuhakikisha miundombinu ya utalii nchini inaimarika na hivyo kuwawezesha watalii wengi kufikia kwa urahisi vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Aidha, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kufadhili mradi huo wenye lengo la kuendeleza shughuli za utalii katika hifadhi za kusini.
“Upatikanaji wa vifaa hivi utapelekea hifadhi hizi kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuendeleza shughuli za uhifadhi pamoja na kuimarisha miundombinu ya utalii na hatimaye kutimiza lengo la serikali la hifadhi zote kuchangia uchumi wa nchi yetu kupitia Utalii,” alisisitiza Mwakilema
Awali, akikitoa taarifa ya makubaliano hayo, Mratibu wa Mradi wa REGROW kutoka TANAPA Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Betrita Lyimo, ametaja idadi ya magari na mitambo 44 itakayonunuliwa kuwa ni pamoja na; Water bowser 5, Fuel bowser 2, Tipper dump truck 17, Concrete mixer 5, Low loader +trailer 2, Expedition truck 3, Mobile workshop 5, Cinema van 4, na Minibus 1.
Mitambo mingine ni Trekta 7, Mower machine za Trekta 6, Water bowser za trekta 8, na trela za trekta ( tani 59)
Maeneo makubwa yatakayoshughulikiwa ni ukarabati wa barabara zipatazo kilomita 2050 hifadhini, kujenga majengo ya watumishi pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja 14 vya ndege vilivyoko kwenye maeneo husika, pamoja na matengenezo ya mitambo na magari.
Mwandishi Wetu,Arusha