MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kutokana na mahitaji ya umeme kwa Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), wameanza mchakato wa kuongeza kwa haraka laini nyingine ya umeme kutoka Kunduchi Dar es Salaam hadi Mtoni Zanzibar.
Amesema hatua hiyo inatokana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuhusu uchumi wa buluu ambao unahitaji matumizi makubwa ya umeme kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji.
Msigwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), aliyasema hayo, katika ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni, mjini Unguja, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo yanayofanywa na serikali.
Alisema umeme utakaopitishwa Zanzibar ni megawati 200 ambao utaongeza matumizi ya umeme kutokana na sera ya serikali ya ujenzi wa viwanda, hivyo mahitaji ya umeme yameongezeka.
Alisema ZECO ni shirika kubwa linalochangia mapato ya TANESCO kwa kiasi cha sh. bilioni 91.7 kwa mwaka.
Msigwa alisema TANESCO imeendelea kuihudumia vizuri ZECO kupitia njia za umeme zilizovushwa baharini kutoka Kunduchi hadi Zanzibar, ambapo kuna laini mbili za msongo wa kilovolti (132KV) (marine cable) ambayo ya kwanza ina uwezo wa megawati 50 na ya pili megawati 100.
Akizungumzia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, nchini Ufaransa, alisema ziara hiyo itazidi kutanua wigo wa maendeleo katika sekta mbalimbali baada ya kushuhudia utiajia saini wa mikataba ya kimkakati.
Alisema katika ziara yake hiyo, Rais Samia pamoja na kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na serikali uliojadili namna ya kunufaika na rasilimali za bahari, Rais Samia pia alishuhudia utiwaji saini mikataba na makubaliano sita kati ya Tanzania na Ufaransa.
Akiitaja mikataba hiyo alisema ni pamoja na mkataba wa ufadhili, maendeleo na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kipaumbele kwa Tanzania, kama vile miradi mikubwa kama SGR na Bwawa la Julius Nyerere.
Mkataba mwingine alisema ni wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milion 178 kwa ajili ya kugharimia mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya tano jijini Dar es Salaam, ambayo itahusisha barabara ya Mandela kwenda Gongola mboto.
Msigwa alisema mkataba mwingine ni wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milion 80 kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kifedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Alisema mkopo huo utafikia malengo ya kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu katia sekta ya kilimo, ambapo wakulima wadogo watanufaika.
Aidha, alisema mkataba mwingine ni wa msaada wenye thamani ya Euro milioni moja kwa ajili ya kuimarisha benki ya maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kufikia malengo ya kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta ya kilimo.
Kwa mujibu wa Msigwa, Rais Samia pia alishuhudia tamko la nia kati ya Rais wa Ufaransa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya ushirikiano katika eneo la uchumi wa buluu na usalama wa bahari.
Aidha, alishuhudia pia tamko la nia kati ya Rais wa Jamhuri ya Ufaransa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya ushirikiano katika miundombinu ya usafiri na maendeleo endelevu nchini.
Akizungumzia Muungano, Msigwa alisema Muungano wa Tanzania umeendelea kuwa imara, ambapo Watanzania wana uhuru wa kufanya shughuli zao katika pande zote mbili ambazo ni Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha alisema, hoja 11 kati ya 18 za muungango tayari zimeshapatiwa ufumbuzi na kwamba hoja zilizobaki zinaendelea kujadiliwa nazo zitapatiwa ufumbuzi.
Na HANIFA RAMADHANI, Zanzibar