KAIMU Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael, amesema usafirishaji wa nyama ya ng’ombe kimataifa umeongezeka hadi kufikia tani 2,000 katika kipindi cha miezi minne.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara.
Michael aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano wa jamii ya wafugaji wa ng’ombe wa kisasa uliofanyika mjini Morogoro.
Alisema baada ya agizo la Rais Samia, timu ya wataalamu wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilipitia upya tozo zote kwa pamoja, ambapo hivi sasa kibali cha kusafirisha na kuuza nyama ya ng’ombe kimataifa ni sh. 40,000 bila kujali thamani ya mzigo wa mfanyabiashara.
Alitaja tozo nyingine kuwa ni ya bodi ya nyama ambayo ilikuwa ukipeleka nyama nje ya nchi, unatozwa asilimia moja ya mzigo uliosafirisha.
“Kwa hiyo lengo letu ni kupata fedha nyingi za kigeni kutokana na mauzo katika masoko ya nje ya nchi, hivyo tulibaini kuweka tozo nyingi kulizuia biashara ya nyama ya ng’ombe nje ya nchi,” alieleza.
Kwa mujibu wa Michael, kipindi cha mwaka jana taifa lilipeleka tani 1,700 za nyama katika mataifa mbalimbali, lakini baada ya kupunguza tozo kumekuwa na ongezeko la upelekaji nyama ya ng’ombe kwa kipindi kifupi hadi kufikia tani 2,000 kwa miezi minne.
Naye, Mkufunzi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Profesa Martin Shem, aliiomba serikali kuwekeza ujuzi na utaalamu wa ufugaji wa ng’ombe kwa kundi la vijana ili kuimarisha ufugaji nchini.
Alifafanua kuwa kundi kubwa la wafugaji nchini ni watu wazima na wazee, hivyo bila ya kuwa na mkakati maalumu wa kuhamasisha ufugaji kwa vijana taifa litafikia kipindi linaweza kuagiza nyama na hata mayai kutoka nje ya nchi.
Profesa Shem alisema taifa limebarikiwa kuwa na maeneo makubwa ya malisho na ya kutosha kwa ufugaji, hivyo liwekeze nguvu kubwa katika kuwarithisha vijana ufugaji.
Mwenyekiti wa jamii ya wafugaji wa ng’ombe wa kisasa, Naweed Mulla, alisema lengo la mkutano huo ni kukutanisha wadau wa ufugaji wa ng’ombe kisasa na serikali kuzungumzia kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji.
“Kupitia mkutano huu wa wafugaji wa kubwa wa ng’ombe tutawasilisha changamoto zetu za wafugaji kwa pamoja kwa zinafanana,” alisema.
Na Scolastica Msewa, Morogoro