SERIKALI ya Tanzania na Ufaransa, zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo ya kimkakati ikiwemo nishati, elimu, kilimo na miundombinu ambapo Ufaransa imekubali kukarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ‘Terminal Two’ Jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, wakati akizungumza na Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Franck Riester, alipowasili Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Alisema kuna miradi ambayo Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali katika sekta tofauti nchini zikiwemo za nishati, wlimu, kilimo na miundombinu.
“Mtakumbuka kuwa Ufaransa ndiyo waliojenga Uwanja wa Ndege wa “Termirnal Two” wa Julius Kambarage Nyerere sasa wanakuja na mradi wa kukarabati uwanja huo na kuufanya kuwa wa kisasa zaidi.
“Sasa hivi ‘Terminal Three’ lakini ‘Terminal Two’ imekuwa ikitumika na ndege zinazofanya safari zake za ndani nchini…Mradi huu ni moja kati ya mradi mkubwa na utakamilika hivi karibuni,”alisema.
Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Riester yupo nchini kuzindua safari za Shirika la ndege la Ufaransa kutoka Paris hadi Zanzibar ambapo mara ya mwisho shirika hilo kufanya safari zake ilikuwa mwaka 1974.
Septemba 15, mwaka hii, Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaouvi alisema Serikali ya Ufaransa kupitia shirika hilo linatarajia kuanzisha safari mpya ya ndege kutoka Ufaransa moja kwa moja hadi Zanzibar kuanzia jana.
Wakati huohuo, Balozi Mulamula alitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Colin Powell.
“Kwa kweli Serikali ya Tanzania tumeshtushwa na kifo chake………katika kipindi chake aliendeleza uhusiano wa Marekani na Mataifa mbalimbali, kwa kweli ni masikitiko makubwa tutamkumbuka daima,” alisema.
Na Mwandishi Maalumu