SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF), limeidhinisha malipo ya Dola za Marekani milioni 567.25 (sawa na sh. trilioni 1.315), kwa serikali ya Tanzania, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa virusi vya corona (uviko-19).
Fedha hizo zinajumuisha mkopo nafuu usio na riba kupitia dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) wa Dola za Marekani milioni 189.08, na mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument (RFI) wa Dola za Marekani milioni 378.17.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango, fedha hizo zitatumika ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022, katika kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na uviko-19.
Ilizitaja sekta zitakazonufaika kulingana na makubaliano na IMF ni afya, elimu, utalii, maji, na kusaidia kaya maskini kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii (TASAF) na kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
“Kila sekta itatumia fedha hizo katika masuala yanayolenga kukabiliana na athari za uviko-19 ambapo pamoja na mambo mengine, sekta ya afya itanunua dawa na vifaa tiba na kugharamia utekelezaji wa mpango wa chanjo,” iliandika taarifa hiyo.
Iliongeza sekta ya elimu itaweka mazingira yatakayowezesha wanafunzi kujifunza bila msongamano na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maboma ya shule na kuongeza madawati.
Hata hivyo, taarifa hiyo inamefafanua kuwa, sekta ya maji itaongeza miundombinu itakayowezesha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wingi mijini na vijijini, huku mpango wa TASAF unaoendelea kutekelezwa utaongezewa fedha ili kusaidia kaya maskini zilizoathirika na uviko-19.
Aidha, inaeleza kwamba, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itawezeshwa kukabiliana na athari za ugonjwa huo, katika sekta zilizoathirika ambazo ni afya, utalii na kilimo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amezisihi sekta zitakazopata fedha hizo kuzitumia kulingana na mpango ulioandaliwa kwa pamoja na sekta husika wa kukabiliana na athari za uviko-19 (TCRP).
“Fedha hizo zitumike kwa kuzingatia makubaliano yetu na IMF kama ilivyoainishwa katika barua ya dhamira ya serikali, ikiwa ni pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati,” amesema.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji ambaye ndiyo Mwenyekiti wa Bodi ya IMF, Bo Li, amesema “Ugonjwa huo umeshoofisha uchumi wa Tanzania”.
SAMIRA OMARY (TUDARCo) Na JUMA ISSIHAKA