SERIKALI kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) imeendelea kuwezesha walengwa kutekeleza miradi mbalimbali ambapo katika kijiji cha Handali Wilayani Chamwino mkoani Dodoma wamejikita katika kutekeleza mradi wa zao la Zabibu na kwa vikundi na mmoja mmoja huku wakieleza kuimarika kwa soko la zao hilo ndani na nje ya nchi.
Mtendaji wa Kata ya Handali iliopo Wilayani Chamwino, Khalfan Myagila, ameeleza hayo Wilayani humo wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya shamba la Zabibu la walengwa wa TASAF lililopo Kata hiyo.
Mtendaji huyo amefafanua kuwa walengwa wamenufaika na soko la zao hilo kutoka kwa wanunuzi wa nje na ndani ya nchi ambapo kwa sasa wanauza sh 1,500 kwa kilo badala ya sh 1,000 kama ilivyokuwa awali.
Mayagila amesema hivi sasa wanauhakika na soko la zao la zabibu kwa sababu kuna wanunuzi wanatoka Kenya na wengine kutoka katika viwanda mbalimbali hapa nchini.
Amesema kwa msimu huu wana uhakika na soko la Zabibu kwa sababu mazao yanastawi vizuri na wamepata wanunuzi wengine wapya ambao wameleta ushindani unaonekana kulingana na bei ambazo wananunua.
“Mradi wa shamba la zabibu uliletwa na walengwa ambapo ulianza 2016 shamba hilo likiwa na Ekari mbili na nusu,ambapo walianza ku himba mitaro kabla ya kuendelea na masuala mengine,”amesema Mayagila.
Mtendaji huyo amebainisha kuwa msimu huu wanatarajia kuvuna Zabibu nyingi ambazo wataziuza na fedha zitakazopatikana zitatumika kufanya maendeleo mbalimbali ya walengwa.
Akizungumza kuhusu mradi huo mlengwa wa mpango wa TASAF Damalis Mtagwa amesema wanaishkuru TASAF kutokana na kwamba imewasaidia kwa kiasi kikubwa kujiinua kiuchumi na kupiga hatua katika kujitegemea.
“Kilimo cha Zabibu kimewasaidia walengwa wengi wa sababu ni cha muda mrefu lakini ukianza kuvuna kila msimu lazima ujiandaa kuvuna zao la hilo,”amsema Mtagwa
Amesema shamba hilo limekuwa shamba la mfano na darasa kwa walengwa wa TASAF, na kila mlengwa baada ya kujifunza aliamua kutoka na kwenda kuanzisha mashamba yao mengine na yanakwenda vizuri.
“Tunashukuru TASAFA imekuwa msaada mkubwa kwetu na kutuwezesha kujikwamua n umasikini, sisi Wananchi na walengwa tumeweza kujiinua kiuchumi kwa kupitia fedha za nguvu kazi ambazo zinatolewa kupitia mpango wa kunusuru Kaya Maskini TASAF,”amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Wilaya ya Chamwino, Mbegu Yange, akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo, amesema walengwa wamekuwa wakifundisha namna nzuri na yenye tija katika magumu ya fedha wanazopewa ili ziweze kuleta manufaa makubwa hapo baadae.
Mratibu huyo amesema wengi wao wamekuwa wakishika vizuri elimu wanayopewa hivyo imepelekea walengwa kuwa vizuri katika kuanzisha biashara ndogo kupitia fedha hizo ambazo zinawakwamua kiuchumi.
Yange amefafanua kuwa walengwa wengi wamepiga hatua kubwa ambapo wanafikiria kuendelea kuwa wajasiriamali wakubwa na kutoka katika mpango huo ili kuwaachia walengwa wngine nao wajiunge na mpango huo.
“TASAF hawachoki na hawatachoka kutoa elimu kwa walengwa kwa sababu lengo lao ni kuhakikisha kila mmoja anapokea fedha na kuzifanyia kitu cha maana cha kujiendeleza kwa sababu TASAF sio ya kwao milele kuna siku walengwa hao watatoka na kuingia wengine,”amesema.
Na Happiness Mtweve, Dodoma