KATIKA kuondokana na changamoto ya kushindwa kuhudhuria masomo kipindi cha hedhi jambo linalotajwa kuwarudisha nyuma Taaluma, shirika lisilo la kiserikali la Victoria Foundation kupitia mradi wa Binti ng’ara, Timiza Malengo yako, limetoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wanaosoma shule zilizopo mkoani Simiyu.
Akizungumza baada ya kukabidhi taulo hizo , mkurugenzi wa shirika hilo Vicky Kamata, amesema kuwa wamepata msukumo wa kutoa msaada huo kutokana na baadhi ya watoto wa kike kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na kutohudhuria kikamilifu vipindi vyote darasani kwa kukosa taulo hizo.
Aidha, Kamata ametoa ombi kwa serikali kuangalia utaratibu wa namna ambavyo shirika hilo linaweza kushirikiana na SIDO ili kutengeneza taulo za kike ambazo zitawasaidia wanafunzi hususan waliopo vijijini.
Nao baadhi ya wanafunzi wamelipongeza shirika hilo kwa msaada huo huku wakisema changamoto kubwa ni kukosa masomo kwa kukosa uwezo wa kununua taulo hizo na kusababisha wengi wao kukaa nyumbani mpaka watakapo kuwa vizuri.
“Unakuta msichana anashindwa kuhudhuria siku saba anakaa nyumbani tu mpaka atoke mwezini..wengine wapata aibu baada ya kutumia vitu visivyo sahihi uchafuka na kuzomewa kiukweli huwezi kuwa na ujasiri wowote ukichekwa” amesema Magreth Sonda, Mwanafuzi kutoka Simiyu sekondari .
Awali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amewataka wanafunzi kufanya jitihada na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao bila kujali mazingira na changamoto wanazozipitia, huku akisisitiza kuwa ipo haja ya kuwasaidia watoto wa kike kupata taulo za kike hususan wale waliopo vijijini.
Na Anita Balingilaki, Simiyu