MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema kuanzia leo itaanza mkakati wa kukomesha tabia ya wafanyabiashara kutotoa risiti za kielektroniki za EFD na wateja kutodai risiti kupitia kampen ya ‘Kamata Wote’.
Imesema hatua hiyo inalenga kujenga tabia kwa wafanyabiashara na wateja kudai na kutoa risiti hizo wanapouza au kununua bidhaa na kukomesha vitendo vya baadhi yao wenye nia ovu ya kuikosesha nchi mapato.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, amesema shabaha ya kampeni hiyo ni kuhakikisha mteja na mfanyabiashara wanatimiza wajibu wao wa kutoa na kudai risiti.
Ameeleza kwa mujibu wa sheria, mfanyabiashara atakayebainika kukwepa kutoa risiti kwa njia yoyote atatozwa faini ya kuanzia sh. milioni tatu hadi sh. milioni 4.5 kulingana na bei ya bidhaa aliyouza.
Amefafanua mbali na faini, mfanyabiashara atakayetenda kosa hilo kwa kujirudia atapelekwa mahakamani na hatimaye kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini kwa pamoja.
Ameongeza adhabu hizo ni kwa mfanyabiashara anayestahili kuwa na mashine ya EFD lakini hajanunua, aliyenayo lakini hatumii, anayetoa risiti za udanganyifu na kwamba ataadhibiwa kwa kila tukio.
Kwa mujibu wa Kayombo, mfanyabiashara anayestahili kuwa na mashine ya EFD ni yule mwenye mauzo ghafi yanayofikia sh. milioni 11 kwa mwaka.
Kwa upande wa mteja asiyedai risiti, amesema atatozwa faini kuanzia sh. 30,000 hadi sh. milioni 1.5 endapo atabainika kutodai risiti kwa mzigo alionunua.
Amesema mbali na kutodai risiti mteja huyo atakumbwa na adhabu hiyo iwapo, atapokea risiti yenye taarifa za uongo ikiwemo isiyolingana bei halisi ya bidhaa aliyonunua.
“Tunachofanya ni kujenga tabia ya watu kutoa na kudai risiti na atakayekumbwa na adhabu hizi ni yule mwenye nia ovu ya kuikosesha nchi mapato, atakayefuata sheria hataadhibiwa,” amesema.
Aidha, amebainisha kuwa, kabla ya kuanza kampeni hiyo, TRA imekuwa ikitoa elimu kuhusu umuhimu wa kutoa risiti kwa wafanyabisahara na kudai risiti kwa wateja tangu mwaka 2010, ambapo mashine za EFD zilianza kutumika.
“Hili jambo linafahamika anayesema hajawahi kusikia anasema hawezi kutoa au kudai risiti kwa sababu hajaelimika, huyo atakuwa na nia ovu na serikali yetu,” amesema.
Ameeleza kampeni hiyo inayoanza kesho Februari 1, 2022 inafanyika nchi nzima na kwamba Mameneja wa TRA, Wilaya wameagizwa kushirikiana na ofisi za Mikoa na Wilaya kufanikisha hilo.
Kayombo amesema wamejipanga vyema kukabiliana na yeyote atakayetumia kampeni hiyo kama mwanya wa kufanya uhalifu, akisisitiza kwamba wapo macho muda wote.
JUMA ISSIHAKA NA REHEMA MOHAMMED