SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limesema linajivunia kuwa chachu ya utoaji huduma za mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambapo linaumiliki kwa zaidi ya asilimia 97 katika data za mawasiliano.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kifurushi kipya cha ‘Bufee Pack’ cha TTCL, Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa shirika hilo, Vedastus Mwita, alisema wanauza data katika nchi kadhaa za ukanda huo.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo ni Rwanda, Burundi, Malawi, Msumbiji na kusisitiza shirika hilo linajivunia kuhakikisha nchi za ukanda wa SADC zinawasiliana kwa kutumia data zake.
Aidha, akifafanua kuhusu kifurushi cha Bufee Pack, Mwita alisema kitakuwa chachu ya kukuza huduma za mawasiliano kwa Watanzania hasa wanaotumia mtandao huo.
Alieleza kifurushi hicho humwezesha mteja kujipangia kiwango cha huduma anachohitaji kulingana na fedha aliyonayo katika simu yake.
“Sisi tumekuja kufuta ule utaratibu wa mtu akiwa na kiasi kidogo cha fedha hataweza kuwasiliana, kifurushi hiki kinampa mteja haki ya kujichagulia kiwango cha huduma anachohitaji, hata akitaka kujiunga MB moja na SMS moja inawezekana,” alisema.
Aliongeza kuwa kuanzishwa kifurushi hicho kumelenga kurahisisha huduma za mawasiliano kwa Watanzania, pia kutoa zawadi kwa wateja kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa nchi na kumalizika kwa mwaka 2021.
“TTCL tunaondoa utaratibu wa kumpangia mteja bei ya kifurushi, akijiunga na Bufee Pack mwenyewe atachagua huduma kulingana na kiasi cha fedha alichonacho hata kiwe kidogo kiasi gani atapata huduma,” alisisitiza.
NA JUMA ISSIHAKA