KUELEKEA siku ya wanawake duniani Chama cha Wanawake wenye viwanda na biashara (Tanzania Women Chamber of Commerce-TWCC) kinaanda maonyesho ya bidhaa na utoaji tuzo kwa wajasiriamali wa viwanda na biashara.
Maonyesho hayo yatafanyika Machi 3 hadi 8 mwaka huu katika Viwanja vya Mnazi Moja, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema utoaji tuzo utafanyika Machi 9 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
“Lengo la maonyesho haya na tuzo ni kuhamasisha wajasiriamali kuongeza nguvu katika kazi zao, pia kukuza uchumi wa taifa kupitia kazi wanazozifanya,” amesema.
Pia, Mwajuma amesema utoaji tuzo hizo ni kusherekea mafanikio wanayoyapata wanawake katika sekta ya viwana na biashara.
“Tuzo hizi zilizunduliwa rasmi Januari 29 mwaka huu kupitia mkutano wa mwezi wa wajasiriamali ulifanyika hapa Jijini Dar es Salaam,” amesema.
Mwenyekiti wa TWCC, Merry Sila, ameeleza kuwa tuzo hizo zinalenga kuonesha mchango wa mwanamke mjasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii.
Ameongezea kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii yoyote, pia wanaweza kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara.
“Naishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ambapo wanawake wengi wameanzisha biashara na viwanda vidogo ambavyo vimeongeza kipato, kuzalisha ajira pamoja kuchangia katika kukua kwa uchumi wa nchi,” amesema.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la TradeMark East Afrca (TMEA), Monica Hangi amesema wametenga shilingi bilioni nne kufanikisha mradi huo wa kujengea uwezo wanawake wa Tanzania kufanya biashara.
“TMEA inafanya kazi na wadau mbalimbali katika kukuza biashara kikanda na kimataifa, tulimua kudhamini tuzo hizi na itandelea kuwa mdhamini mkuu kutokana na lengo kubwa ni kuhakikisha biashara za wanawake zinakuwa na kuleta tija kwa taifa,” amesema.
Na AMINA KASHEBA