MAHAKAMA Kuu Divesheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu Mahakama ya Mafisadi, inatarajia kutoa uamuzi Septemba 6, mwaka huu wa mapingamizi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi, katika kesi ya uhujumu uchumi, yenye mashitaka sita, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Jaji Elinazer Luvanda, alisema hayo mahakamani, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya upande wa mashitaka kujibu hoja za mapingamizi yaliyotolewa na upande wa utetezi.
Awali, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala, uliwasilisha mapingamizi matatu, ikiwa ni pamoja na sheria ambayo imetumika kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, akidai kuwa haitoi tafsiri ya neno ugaidi na pia haijasema lengo la ugaidi wanaotuhumiwa nalo kama ni la kidini, kisiasa au kijamii.
Katika pingamizi hilo pamoja na mambo mengine, walidai sheria ya ugaidi ambayo wanashitakiwa nayo haijafafanua viambato vya kosa la ugaidi, na kwamba upande wa mashitaka haujazingatia masharti ya lazima ya sheria hiyo ambayo ni kueleza kusudio la vitendo vya ugaidi ambavyo washitakiwa wanatuhumiwa kutenda.
Hata hivyo, mawakili wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando, wakijibu hoja za utetezi, walipinga vikali pingamizi hilo wakidai hoja zao hazina mashiko.
Walidai hati ya mashitaka iko sahihi na haina kasoro hizo zinazodaiwa na upande wa utetezi, huku wakisisitiza kuwa sheria haina kasoro, na kwamba hati ya mashitaka imekidhi matakwa ya kisheria pamoja na kutoa taarifa ambazo zinawawezesha washitakiwa kufahamu makosa wanayoshitakiwa.
Hivyo waliiomba mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo ili kesi hiyo iendelee kusikilizwa katika hatua ya awali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Jaji Elinazer Luvanda, anayesikikiza kesi hiyo aliahirisha hadi Jumatatu kwa ajili ya uamuzi wa pingamizi hilo.
Upande wa mashitaka unawakilishwa na jopo la mawakili wa serikali watano, huku upande wa utetezi ukiwa na mawakili zaidi ya 14 wakiongozwa na Peter Kibatala.
Akijibu hoja ya tatu ambayo ilitolewa na upande wa utetezi, wakili Kidando alidai suala la upande wa utetezi kutaka hati ionyeshe malengo ya ugaidi huo kisiasa kijamii na kidini haina mashiko.
Wakili Kidando alidai katika sheria ya ugaidi, inatoa mlolongo wote wa makosa ya ugaidi na kwamba wao kuna kanuni zinazowaongoza katika kuandaa hati ya mashitaka na hizo zinawasiadia washitakiwa kujua aina ya kosa ambalo wamelitenda.
Pia, alidai katika sheria za Tanzania hakuna mahali ambapo inaainisha lengo la ugaidi, ambapo wao hawajatumia sheria za hapa nchini, bali zimechukuliwa kutoka katika nchi nyingine, hivyo msingi wao uliotumika katika kuleta mapingamizi hayo mahakamani hauna msingi.
Katika mapingamizi mengine upande wa utetezi unadai katika hati ya mashitaka kifungu cha 4 kidogo cha 1 cha sheria ya ugaidi, hakijatoa maana ya ugaidi hivyo kina upungufu.
Akijibu hoja hiyo, wakili Kidando alidai katika sheria za kimataifa hakuna mahali ambapo imetoa tafsiri ya ugaidi bali katika kifungu cha 4 (2) cha sheria ya ugaidi, inatoa tafsiri ya vitendo ambavyo mtu akifanya vinajulikana kama ugaidi.
Hivyo, kwa kuzingatia sheria hizo, hoja hizo zote hazina mashiko na kuiomba Mahakama itupilie mbali mapingamizi hayo.
Baada ya upande wa mashitaka kujibu hoja hizo upande wa utetezi nao walipewa tena nafasi, ambapo waliendelea kuonyesha msisitizo wao kwamba hati ya mashitaka ina upungufu.
Akiendelea kuweka mapingamizi, wakili Kibatala, alidai hati ya mashitaka haijaonyesha kusudio la vitendo vya ugaidi pia sheria ina upungufu kwasababu haijatoa tafsiri ya neno ugaidi.
Agosti 31, mwaka huu, upande wa utetezi uliwasilisha pingamizi moja la kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya ugaidi kwa kuwa ni mahakamani ya mafisadi.
Walidai kesi ya ugaidi inatakiwa kusikilizwa Mahakama Kuu na siyo ya mafisadi na baada ya pingamizi hilo Septemba Mosi, mwaka mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo.
Baada ya kutupilia mbali pingamizi hilo, siku hiyo wakawasilisha mapingamizi mengine, ambapo upande wa mashitaka walijibu mapingamizi hayo na kisha Jaji Luvanda akapanga kutoa uamuzi Septemba 6, mwaka huu.
Mbali na Mbowe, ambaye ni mshitakiwa wa nne, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adamu Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Ling’wenya.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka sita ikiwemo mawili ya kula njama kutenda makosa ya ugaidi kwa washitakiwa wote.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti Mosi na Agosti 5, mwaka 2020 katika Hoteli ya Aishi, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.
Wanadaiwa walikula njama kwa lengo la kulipua vituo vya mafuta, maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu, katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza na kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro Lengao Ole Sabaya.
Shitaka la tatu ni kufadhili vitendo vya kigaidi linalomhusu Mbowe peke yake.
Na SYLVIA SEBASTIAN