GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga, amesema mwenendo wa uchumi wa ndani Tanzania Bara, umeendelea kuimarika hadi kufikia asilimia 4.7 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021.
Kadhalika, uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa asilimia 6.5 katika robo ya pili ya mwaka 2020, ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.4 katika robo ya pili ya mwaka 2020.
Profesa Luoga amebainisha hayo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ambapo amesema matokeo hayo yamebainishwa na Kamati ya Sera ya Fedha ya BoT, iliyokutana mwanzoni mwa wiki hii.
Katika taarifa hiyo, Gavana alisema kamati imebaini kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imekuwa chini kidogo ya matarajio ya awali yaliyowekwa kidunia.
Alieleza hali hiyo imetokana na kuibuka upya kwa janga la Uviko-19 katika baadhi ya nchi na kupanda kwa bei za nishati duniani.
“Hata hivyo, ukuaji huu wa uchumi wa dunia unatarajia kuchangia kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Tanzania,” alieleza Gavana katika taarifa yake.
Alisema kamati ya sera ya fedha imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha Septemba na Oktoba, mwaka huu, ambao uliwezesha kuendelea kuwepo ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki.
Profesa Luoga alisema hali hiyo ilichangia mwenendo wa riba katika soko la fedha kuendelea kuwa tulivu na katika viwango vya chini.
Gavana huyo alieleza ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, umeimarika kufikia asilimia 4.6 kwa mwaka ulioishia Septemba 2021, kutoka asilimia 3.2, iliyokuwepo Agosti.
Amesema kamati hiyo pia imejiridhisha kasi ya ukuaji wa mikopo katika sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuimarika kwa sababu ya vichocheo mbalimbali.
Mojawapo amesema ni kuimarika uchumi wa dunia na hatua za kisera zilizochukuliwa na Benki Kuu ili kuchochea upatikanaji wa mikopo kwa riba nafuu.
FEDHA ZA KIGENI
Kwa mujibu wa Gavana Luoga, akiba ya fedha za kigeni nchini, imeendelea kuwa ya kuridhisha na kufikia Dola za Marekani bilioni 6.7 hadi kufikia Oktoba, mwaka huu.
Alisema kiasi hicho kinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi saba sawa na lengo la nchi na makubaliano ya jumuiya za kikanda.
MFUMUKO WA BEI
Katika taarifa yake, Gavana alisema mifumuko ya bei duniani, imekuwa ikipanda kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na kupanda bei za nishati.
Hata hivyo, alisema Benki Kuu nyingi duniani zinaona ongezeko hilo kuwa la mpito, hivyo kuendelea na sera ya fedha yenye kuongeza ukwasi katika uchumi.
Alisema mfumuko wa bei uliendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia kati ya 3 hadi 5, sanjari na makubaliano ya kikanda kwa nchi za EAC na SADC.
“Mfumuko wa bei unatarajiwa kusalia sambamba na lengo, licha ya kuongezeka kidogo tangu mwezi Juni 2021,” alieleza Gavana Luoga.
Pia aliongeza kuwa: “Kamati inaamini kwamba kuongezeka uzalishaji wa mafuta duniani kutapunguza kupanda kwa bei ya nishati.”
Alisema pamoja na hayo, kamati inasisitiza umuhimu wa kuendelea kwa upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini na uimara wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni kunakotarajia kupunguza athari ya kupanda kwa bei ya mafuta kwenye mfumuko wa bei.
UKUSANYAJI MAPATO
Gavana Luoga alisema ukusanyaji wa mapato ulikuwa wa kuridhisha, huku mapato ya kodi yakiwa zaidi ya asilimia 90 ya lengo.
Alisema mfumuko wa bei uliendelea kuwa chini ya lengo la asilimia 5, huku ukusanyaji wa mapato ukiwa sawa na asilimia 73.6 ya lengo.
Kwa mujibu wa Gavana, sekta ya nje imeendelea kuimarika kutokana na athari za janga la Uviko-19, ikiendelea kuwa na nakisi ndogo za urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje.
Alifafanua katika taarifa hiyo kuwa, hali hiyo inatokana na kuanza kuingia mapato ya nje ya mauzo ya madini, mazao ya biashara na shughuli za utalii.
Gavana Luoga alisema kwa kuzingatia tathimini ya mwenendo wa uchumi wa hivi karibuni na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia BoT kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwa kipindi cha Novemba na Desemba, mwaka huu ili kuendelea kuimarisha uchumi.
Na WILLIAM SHECHAMBO