OFISI ya Taifa ya Takwimu, imetoa taarifa ya robo tatu ya mwaka unaoishia Septemba 2020/2021, ambapo uchumi umekua kwa asilimia 5.2 kutoka 4.4 kwa mwaka 2020, huku pato la Taifa likiongezeka hadi kufikia sh. trilion 37.0 kutoka trilioni 34.5 kipindi kama hicho mwaka 2020.
Pia, imesema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021, shughuli ya huduma za malazi ya huduma za chakula iliongoza kwa kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa asilimia 14.3, ikifuatiwa na uchimbaji wa madini na mawe (asilimia 12.2) burudani, shughuli za kaya katika kuajiri (asilimia 12.1) umeme (asilimia 10.0) na habari na mawasiliano (asilimia 9.3).
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Daniel Masolwa, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ukujuaji wa uchumi katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka jana.
Alisema pato halisi la Taifa limeongezeka hadi sh.trilioni 32.0 mwaka jana kutoka sh.trilioni 30.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Masolwa alisema katika kipindi hicho cha robo ya tati ya mwaka jana, pamoja na changamoto za Uviko-19 uchumi umeendelea kumairika ambapo shughuli za huduma ya malazi na chakula iliongezeka kwa kiwango cha juu zaidi cha asilimia 14.3 ikilinganishwa na kiwango hasi cha asilimia 25.1 kwa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa Masolwa, ukuaji uliochangiwa na kuongezeka kwa watalii 243,565 walioingia nchini kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2021 ikilinganishwa na watalii 72,147 kipindi kama hicho mwaka 2020.
“Mwaka 2021, katika kipindi cha JanuariMachi, uchumi iliongezeka kwa asilimia 5.0, katika kipindi cha Aprili-Juni uchumi iliongezeka kwa asilimia 4.5 na katika kipindi cha Julai-Septemba uchumi iliongezeka kwa asilimia 5.2 kwa msingi huo, katika kipindi cha Januari-Septemba uchumi iliongezeka wa wastani wa asilimia 4.9,”alisema.
Alisema Wizara ya Fedha na Mipango, ilikadiria uchumi wa Tanzania kuongezeka kwa asilimia 5.0 mwaka jana.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema Shirika la Fedha Duniani (IMF) nalo lilikadiria uchumi wa Tanzania kuongezeka kwa asilimia 4.0 katika mwaka 2021, ikiwa ni tofauti ya pointi za asilimia 1.0 Kati ya makidirio ya Wizara ya Fedha na IMF kutokana na tofauti ya vigezo na methodolojia zilizotumika kwa vyanzo vyote viwili.
Alisema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021, shughuli ya huduma za malazi ya huduma za chakula, iliongoza kwa kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa asilimia 14.3 ikifuatiwa na uchimbaji wa Madini na Mawe (asilimia 12.2).
“Huduma nyingine za jamii zikijumuisha na Burudani na shughuli za kaya katika kuajiri (asilimia 12.1) umeme (asilimia 10.0) na habari na mawasiliano (asilimia 9.3),” alisema.
MCHANGO WA SHUGHULI KUU ZA KIUCHUMI
Alisema mchango wa shughuli kuu za kiuchumi umeainishwa kwa kuzingatia mchanganuo wa shughuli kuu za uchumi. Masolwa alifafanua kuwa shughuli za huduma zilikuwa na mchango mkubwa zaidi wa asilimia 42.1 ya pato la Taifa zikifuatiwa na shughuli za msingi (asilimia 30.1) na shughuli za Kati (asilimia 27.8).
MCHANGO KATIKA UKUAJI
Alisema katika robo tatu ya mwaka 2021, ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.2 uliochangiwa na shughuli zote za uchumi.
“Shughuli zilizokuwa na mchango mkubwa katika ukuaji zilikuwa ni Ujenzi asilimia 18.1, Kilimo asilimia 15.1, uchimbaji wa Madini na Mawe asilimia 11.4, uzalishaji Viwanda asilimia 8.6, Utawala na Ulinzi asilimia 5.8 na Biashara na Matengenezo asilimia 4.0,”alisema.
Alisema kulingana na makadirio ya IFM ya Oktoba 2021, uchumi wa dunia wa mwaka 2021 unaotarajiwa kukua kwa kiwango cha asilimia 5.9 kwa mwaka 2021.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2022 yameendelea kubaki katika kiwango cha asilimia 4.9.
Alisema makadirio ya ukuaji wa uchumi katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara yaliyofanyika Oktoba, mwaka jana, yalionyesha kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi hadi asilimia 3.7 kwa mwaka 2021.
“Makadirio haya yanatarajiwa kuongezeka na kutokana na kuimarika kwa usafirishaji wa bidhaa nje ambazo zimesaidia kukabiliana na madhara ya kuagiza zaidi bidhaa za chanjo ya UVIKO-19 kutoka nje ya nchi,” alisema.
Alisema katika mwaka 2021, uchumi wa nchi za jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika umekadiriwa kukua Hadi asilimia 3.7 . “Katika kipindi cha Julai-Septemba 2021, ukuaji wa uchumi kwa baadhi ya nchi za JUMUIYA YA MAENDELEA KUSINI MWA AFRIKA (SADC)
kama vile afrika Kusini ulipungua Hadi kiwango cha asilimia 1.5 ikilinganishwa na asilimia 13.9 wakati uchumi wa Namibia iliongezeka Hadi asilimia 2.4 kutoka kiwango hasi cha asilimia 12.3 mwaka 2020,”alisema
Alisema katika kipindi cha JulaiSeptemba 2021, uchumi wa nchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), umeendelea kuimarisha kutoka kiwango hasi cha ukuaji hadi kiwango chanya.
Kaimu Mkurugenzi huyo hadi juzi nchi tatu Kati ya Sita zimekamilisha kutayarisha na kusambaza taarifa ya Pato la Taifa.
“Taarifa za Pato la Taifa robo ya Tatu ya watu 2021 zinaonyesha kuwa uchumi wa Rwanda ukiongezeka kwa asilimia 2020, Uganda uchumi uliongezeka kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na kiwango hasi cha asilimia 0.8 kipindi kama hicho mwaka 2020,” asilimia.
Alisema ofisa hiyo inaendelea kutekeleza Sera ya Mapitio ya Takwimu zao Pato la Taifa, ambayo inaruhusu kuchapisha matokeo ambayo yanayoweza kufanyiwa Mapitio kutokana na upatikanaji wa takwimu mpya za robo mwaka na za mwaka mzima.
NA HAPPINESS MTWEVE, Dodoma