BALOZI mdogo wa China Zanzibar, Zhang Zhisheng, amesema ushirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China utaendelea kuimarika kutokana na udugu wao wa muda mrefu, uliopo.
Kauli hiyo ameitoa wakati akikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dk. Omar Dadi Shajak, visiwani humo.
Amesema vifaa hivyo zikiwemo barakoa na mitungi ya gesi ya oksijeni, ni kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, Unguja na Hospitali ya Abdalla Mzee iliyoko pemba.
Balozi huyo amesema ushirikiano wa pamoja unahitajika ili kupambana na wimbi la tatu la Covid-19, ambalo dalili zinaonyesha linaendelea kuathiri duniani kote.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dk. Omar, amemshukuru Balozi huyo kwa kuiunga mkono SMZ kwa vifaa hivyo na kuwapatia mafunzo wataalamu wa afya Zanzibar.
Ameahidi SMZ itaitumia vizuri misaada hiyo ambayo itasaidia katika kupambana na maradhi ya covid-19 kwa wananchi wa Zanzibar .
Katibu Mkuu amesisitiza wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, katika kujikinga na corona kwa kuvaa barakoa,kunawa mikono mara kwa mara na kuepukana mikusanyiko isiyo ya lazima .
Wakati huo huo Dk. Shajak amepokea msaada wa mashine ya kupumulia kutoka kwa Shirika la Japiego kupitia kwa Mkurugenzi wa Afya Laurel Fain kutoka Marekeni.
Na Thabit Madai