WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro, amesema kutokana na udhibiti wa ujangili unaofanywa na Mamlaka ya Uhifadhi ya Wanyama Pori Tanzania (TAWA) ujangili nchini umepungua kwa asilimia 90.
Pia, amesema wizara yake imejipanga mwaka huu wa fedha kutoa tuzo kwa waaandishi watakaofanya vyema katika uhifadhi.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri Dk.Ndumbaro alisema kazi waliyoifanya TAWA ya kudhibiti ujangili si kazi ndogo,
“Unaposemajangilinimtuanayeingia katika maeneo yaliyohifadhiwa na kuna wanyama wakali, lakini mtu anajitoa maisha yake kwa manufaa yake, TAWA wamejitoa kwa faida ya nchi hivyo wanafanya kazi kubwa, ujangili wa nyara umepungua kwa zaidi ya asilimia 90 sasa umebaki ujangili wa kitoweo,”alisema.
Dk. Ndumbaro alisema mamlaka hiyo inafanya kazi kubwa licha ya kuwa taasisi changa, lakini imekuwa ikijitoa kwa maslahi ya taifa.
“Maeneo magumu ya uhifadhi yapo chini ya TAWA na hata mtu yeyote akiyaona hawezi kupita, lakini wao wanafanya kazi, tuna kila sababu ya kuwapongeza, ikolojia imeimarika kwa maeneo wanayosimamia hakuna ukataji hovyo wa misitu, mito mingi inatiririsha maji wakati wa kiangazi sababu ya uhifadhi wa taasisi hii,’’alisema.
Akizungumzia tuzo kwa waandishi wa habari, Dk.Ndumbaro alisema itahusisha waandishi watakaoandika
habari bora zinazohusu uhifadhi. “Tutatoa tuzo kwa waandishi watakaoandika habari za kufichua ujangili na kuhamasisha utalii, tumeanza kufuatilia kuanzia Julai, mwaka huu ili ikifika mwisho wa bajeti mwakani tutoe tuzo kwa waliofanya vyema,”alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Sylvester Mushi, alisema kutokana na taasisi hiyo kubadilishwa kutoka katika muundo wa kiraia kuwa ya kijeshi wamekua wakipata ushirikiano na wananchi katika kudhibiti ujangili.
“Wananchi wanatupa taarifa kwa siri za kiitelijensia na kutufanikisha kuharibu mtandao wa kijangili, pia mamlaka imeongeza vitendea kazi kwa watumishi hatua iliyoongeza morali katika kazi,”alisema Mushi.
NA BARAKA LOSHILAA