CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema serikali ipo katika hatua ya mwisho ya utekelezaji wa Ilani katika ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya urefu wa kilomita 300, kutoka Mtwara Pachani-Lusewa-Nalasi hadi Tunduru.
CCM imesisitiza kuwa inatambua maumivu waliyonayo wananchi kutokana na kuchelewa kwa ujenzi wa barabara hiyo, ambayo ni muhimu katika kuimarisha uchumi.
Kutokana na uwepo wa maeneo korofi katika barabara hiyo, jana Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, alipata ajali ya gari akiwa katika ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya CCM.
Akizungumza katika Kijiji cha Lusewa, wilayani Namtumbo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Christina Mndeme, alisema amejionea kwa macho uhitaji wa barabara hiyo.
“Leo (jana) msafara wangu umepata ajali gari ya mbunge iliingia kwenye shimo na kupinduka mara tatu, tunashukuru Mungu hakuna aliyeumia, nawahakikishia nawasiliana na TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania), waniambie lini wanaanza ujenzi na najua ipo katika Ilani na tathmini imeshafanyika, hivi naagiza ujenzi uanze,” alisema.
Mndeme, alisema wananchi wa maeneo hayo wameteseka kwa muda mrefu kutokana na kero hiyo ya barabara, hivyo ni muhimu wizara husika kuchukua hatua za haraka.
“Hakuna tena cha kusubiri, zaidi ya sh. bilioni mbili zilishatolewa, upembezi yakinifu umeshafanyika ili kulipa fidia wananchi wa pembezoni na tathmini tayari ikiwemo kujua madaraja yanayohitajika, sijui nini kinachelewesha, ninachotaka kusema sitaki kusikia michakato hii barabara ni muhimu,” alisema.
Aliongeza kuwa mbali na barabara hiyo, alimwagiza Meneja wa TARURA wa wilaya, kufika katika Kijiji cha Magazine na Lusewa ili kuharakisha mradi wa umeme.
Alisema kilichofanyika ni kuleta nguzo na kuzitelekeza na wananchi hao hawahitaji nguzo, wanahitaji umeme, ambao haujawahi kufika tangu Uhuru na CCM imeahidi katika Ilani.
Akizungumzia bei ya pembejeo ambayo imelalamikiwa na wananchi hao kuwa kubwa, Mndeme aliahidi kufanyia kazi tatizo hilo na kutaka viongozi wa halmashauri kuharakisha mchakato wa ugawaji wake kwa ajili ya zao la korosho.
Pia, alionyesha kukerwa na hatua ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutolipa fidia, kwa wakulima walioliwa mazao yao na wanyamapori zaidi ya hekta 56.
Alisema anakwenda kufanyia kazi na atawasiliana na waziri husika ili kubaini watendaji ambao kwa makusudi wanataka kugombanisha wananchi na serikali yao.
Pia alisisitiza kuwa atazungumza na Waziri wa Kilimo ili mkoa huo wa Ruvuma uweze kuwekewa kituo cha kuuza mahindi eneo la Lusewa kwa kuwa wanazalisha kwa wingi.
Alisema pia anatambua kero ya wakulima na wafugaji ambapo hakuna mpangilio wa ugawaji wa maeneo, tatizo ambalo linasababisha na viongozi wa eneo hilo na kuzua mgogoro hivyo Chama kitatoa maelekezo.
Kwa upande wa Mbunge wa Namtumba Kawawa, alisema maeneo ya vijiji hivyo vina changamoto ya huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, miundombinu, maji na umeme.
Alisema tatizo la umeme ni kubwa na hakuna hatua zaidi ya kuwekwa nguzo kwa muda mrefu na kijiji cha Ligunga kimerukwa na mradi hivyo wanaomba Chama kuingilia kati.
Na MARIAM MZIWANDA