SERIKALI imesema Ujenzi wa Chuo cha Ufundi kinachojengwa katika eneo la Nala jijini Dodoma utakaogharimu Tsh. Bilioni 17.9, utaleta manufaa katika kuzalisha vijana wenye ujuzi ambao watakwenda kutumika katika viwanda mbalimbali vinavyoendelea kujengwa.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho na Ujenzi wa shule ya Sekondari mfano iliyopo Iyumbu.
Amesema chuo hicho baada ya kukamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 3000.
“ujenzi huu ulianza June mwaka huu na unatarajiwa kumalizika Disemba 2022, ujenzi unaendela vizuri, nchi inakwenda katika viwanda hivyo tumepanga kuzalisha wataalamu wengi katika vyuo hivi” amesema Kipanga.
Ameongeza “Lengo la kujenga chuo hicho ni kuzalisha vijana wengi wenye ujuzi ambao watakwenda kutumika katika viwanda mbalimbali vinavyoendelea kujengwa, kuwezesha vijana wengi kupata ujuzi, kuzalisha vijana wenye ujuzi wa kati, Serikali imejipanga kujenga Vyuo vya Ufundi katika kanda zote ikiwemo kanda ya Kati, kanda ya ziwa, kanda ya Kusini na kanda ya kaskazini,”amesema
Awali Mhandisi Msaidizi kutoka Kampuni ya BICO, Aliki Nziku, amesema mradi huo ni mpango wa Serikali kuongeza Wataalam katika nyanja za ufundi na Teknolojia.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo alitembelea na kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari mfano iliyopo Iyumbu inayojengwa na SUMAJKT kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 17 ambayo inatarajiwa kuanza kuchukua wanafunzi January 2022.
Na Happiness Mtweve,Dodoma