WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi na ubora wa majengo ya Ikulu ya Chamwino, uliofikia asilimia 91 na kumtaka mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika Mei, mwaka huu.
Majaliwa aliyasema hayao baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ikulu inayojengwa katika eneo la Chamwino, Jijini Dodoma.
Aliwasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati na kuwapongeza wote wanaohusika na ujenzi.
“Tunataka kumuwezesha Mheshimiwa Rais kufanya kazi katika eneo lake maalumu na afanye kazi katika mazingira mazuri na kwa ufanisi.
“Nimefurahishwa na taarifa kwamba ujenzi huu umefikia asilimia 91 na hatua iliyobaki hizi asilimia 9 ni kazi ndogondogo kama uwekaji wa milango, njia za mifumo ya hewa na umeme na zote zinaenda vizuri,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan pia anatarajia kuona ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Alilipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza ujenzi huo kwa ufanisi.
“Ramani iliyoko hapa iko sawasawa na jengo la Ikulu lililoko Dar es Salaam. Wakandarasi wetu mmefanya kazi kubwa sana, Hii imedhihirisha kuwa nchi yetu ina wataalam wa kutosha kujenga aina yoyote ya majengo,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mhandisi Daudi Kondoro, alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba mradi huo utakamilika na kukabidhiwa Mei kama inavyotarajiwa kwa kuwa sasa uko hatua za mwisho za ukamilishaji.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
NA MWANDISHI WETU