UKITAKA kuona rangi halisi za Rais Samia Suluhu Hassan, basi thubutu kudokoa shilingi ya serikali. Hayo ndio yamedhihirika baada ya Rais Samia kuagiza wale wote waliobainika kuiba pembejeo za ruzuku zinazotolewa na serikali kwa wakulima,kushughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria.
Rais Samia alitoa onyo hilo jijini Dodoma wakati akizindua ugawaji wa vitendea kazi kwa maofisa ugani nchini, ambapo alisema wapo watu wakisikia neno ruzuku kazi yao ni kwenda kuiba.
“Lakini kwenye hili la pembejeo, nimeona kwenye luninga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila, amekamata watu wanaoiba pembejeo za ruzuku na hii kesi ipo TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa).
Mkuu wa Mkoa, nataka hawa watu wazione zile rangi zangu ninazozizungumza ili wengine wakishazisoma, hawataiiba zile pembejeo kwa sababu wameshazoea kusikia neno ruzuku ni kwamba kazi yake kuliwa, kazi yake vocha feki, kazi yake ni kuziiba. Nataka uwashughulikie sawaswa.
“Nimeambiwa umewakamata walioiba na ruzuku na fedha za ushirika, nataka uwashughulikie kisawasawa na Waziri Mkuu ulisimamie hilo,” aliagiza mkuu wa nchi.
UTOAJI RUZUKU
Akizungumzia utoaji ruzuku kwa wakulima, Rais Samia alisema mwaka jana alitoa maelekezo ya kufanyika majaribio ya kutoa ruzuku za pembejeo kwa wakulima, jaribio ambalo limeonyesha mafanikio kwa kuongeza uzalishaji katika mazao ya pamba, korosho na tumbaku.
Alisema katika majaribio hayo, sh. bilioni 56 zilitumika katika pamba, sh.bilioni 61 ziliingizwa katika korosho na sh. bilioni 32 zikipelekwa katika zao la tumbaku.
ATOA TAHADHARI HALI YA CHAKULA
Rais Samia alitoa tahadhari kwa wakulima kuhakikisha kwamba wanajitosheleza mahitaji ya chakula kabla ya kuuza mazao yao nje ya nchi.
“Nitoe indhari hapa, tuangalie na hali ya chakula nchini kwa sababu kutokana na mabadiliko ya hali ya uchumi duniani na janga la Uviko-19, chakula ni mahitaji makubwa sana. Tunaweza tukavutika sana na soko la dunia tukajisahahu kuweka akiba nchini. Niombe sana tujitosheleze kwanza nchini halafu tusafirishe tupeleke kwa wenzetu,” alieleza.
Alisema utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta ya kilimo ikiwemo uzalishaji na biashara ya mazao ya kilimo, na upatikanaji wa huduma muhimu kama mbegu, mbolea na viwatilifu hutegemea mchango na ushiriki wa sekta binafsi.
Hivyo, aliiomba sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kilimo, badala ya kuongeza ujuzi ambao wapo wataalamu wenye uweledi.
“Kwa hiyo misaada tutakayoipata ijielekeze kwenye uwekezaji katika miundombinu au huduma za kilimo. Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza shughuli za maendeleo pamoja na washirika wa maendeleo wanaounga mkono jitihada za serikali kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo,” alibainisha.
Rais Samia aliiagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo kushirikiana katika kuirejesha Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya kilimo, ukiwemo mradi wa “Feed for Future.”
“Nimesema mradi huu makusudi kwa sababu waziri amesema dunia inakwenda kuongeza idadi ya watu lakini, mabadiliko ya kiuchumi yaliyoletwa na Uviko-19 yamebadilisha mwelekeo wa kiuchumi. Mazao ya kibiashara na mazao yale tuliyosema ya chakula, sasa yote ni mazao ya kibiashara.
“Watanzania hatukuwaza hata siku moja kwamba mchele wetu tutaukuta katika maduka ya kisasa ya Ulaya, Parachichi zetu tutazikuta Ulaya, nyama ya Tanzania inatakiwa kote Ghuba ya Uarabuni na Ulaya, kwa hiyo kila kitu kinachozalishwa Tanzania ni zao la biashara, hatuna budi kubadilisha mwelekeo wa sekta ya kilimo,” alieleza.
Aliongeza kuwa: “Ndio maana ya ajenda kwamba ifikapo 2030 sekta ya kilimo iwe imekuwa kwa asilimia 10 tuweze kuchangia mahitaji ya chakula duniani, tuna fursa nzuri tumezalisha lakini bei za dunia zimetuvuta nyuma, tumekwenda na kilimo tumechechemea. Sasa hivi mabadiliko ya uchumi wa dunia yanatupa fusra Tanzania tuzalishe kwa wingi ili tutumie soko la dunia kwa bei ambazo sisi tunaopeleka mazao yetu na sio kupangiwa bei na wao.”
Mkuu wa nchi alisisitiza, “Niwaombe sana vijana wa Tanzania ingieni kwenye sekta hii, hamtojuta. Mtatengeneza pesa ya halali mikononi mwenu, nikuombe waziri vile vizimba mnavyotengeneza mikoani, tengeni vingine kwa ajili ya vijana, wakuu wa mikoa na wilaya mshirikiane katika hilo,” alibainisha.
WAZIRI MKUU
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema ili kupatikane mafanikio ya kiuchumi lazima Tanzania ijikite katika sekta ya kilimo na ndio sababu Rais Samia amekuwa akitoa maelekezo muhimu, yenye kusisitiza wakulima kulima kilimo chanye tija.
Akizungumza katika hafla hiyo ya ugawaji wa vitendeakazi kwa maofisa ugani, Majaliwa alisema asilimia 60 ya Watanzania wamejikita katika sekta ya kilimo.
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020 hadi 2025 iliweka mkazo kusimamia sekta ya kilimo, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa maelekezo na mimi nimekuwa nikiyabeba huku akisisitiza wakulima kufanya kilimo chenye tija,”alisema Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa: “Naomba nirejee kauli yake ambapo alieleze ili kupata mafanikio ya kiuchumi katika nchi hii lazima kujikita katika kilimo, kwa sababu asilimia 60 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, kama kusipoweka mkazo kwa Watanzania hawa maana yake muda wote watakuwa wakilalamikia serikali.”
Alibainisha kuwa Tanzania inatumia zaidi ya sh. bilioni 470 kwa mwaka, kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi.
Alisema ili nchi ijitosheleze kwa mafuta, serikali ilianza kugawa miche ya michikichi na kufanya hamasa ya kilimo cha alizeti katika mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara lengo likiwa kuongeza uzalishaji.
WAZIRI WA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema sekta ya kilimo haiwezi kubadilika kama hatua hazijachukuliwa kwani kuna uhusiano kati ya ukuaji sekta ya kilimo na pato la taifa, hivyo kilimo kikianguka na pato la taifa linaanguka.
“Hii ni tafsiri halisi ya umuhimu wa sekta ya kilimo hapa nchini, kwa ajili ya kukuza pato la taifa, taifa letu lina eneo la kilimo lenye ukubwa wa hekta milioni 44, ambapo hekta milion 29 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji,” alisema.
Alisema hadi kufika mwaka 2030, Tanzania inakadiriwa itakuwa na watu milioni 100, hivyo nchi itakuwa na uwezo wa kuwa kitovu cha chakula kwa nchi za Afrika.
“Ili kufikia malengo hayo kama nchi tumeamua kwenda na mambo saba uliyoyasema wakati ukilihutubia Bunge, Aprili mwaka jana, ambapo ulisisitiza kilimo chenye tija. Kwa kulitekeleza hilo tulianza kufanyia kazi katika kuweka nguvu kubwa kwenye utafiti,” alisema.
Alisema wizara imejipanga hadi kufikia mwaka 2030 sekta ya kilimo ikue kwa asilimia 10 kwa miaka 10 mfululizo, ambapo itasaidia kupunguza idadi ya watu ambao bado wapo kwenye mstari wa umaskini.
MUSSA YUSUPH NA FRED ALFRED, DODOMA