NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema wafugaji wanaoingiza mifugo yao kulisha katika mashamba ya wakulima, ni wahalifu na lazima wachukuliwe hatua za kisheria.
Ulega aliyasema hayo wakati wa ziara ya kutatua migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi aliyoifanya Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani Novemba Mosi, mwaka huu.
“Ikiwa mtu amevamia shamba la mwenzie na mifugo yake ikala mazao katika shamba hilo, hapo hakuna kupindisha maneno, ni lazima haki itendeke, achukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kumfidia yule ambaye mazao yake yameliwa na mifugo,” alisema Ulega.
Ulega alitumia nafasi hiyo pia kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi ya dhati, kusimamia utatuzi wa migogoro hiyo kwa nia ya kutunza amani na utulivu katika wilaya hiyo na nchi kwa ujumla.
Pia alishauri uongozi wa wilaya kuunda kamati maalumu za maridhiano zitakazoshughulika na utatuzi wa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ili waishi kwa amani na kushirikiana.
Aidha, alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir kuhakikisha anaratibu vizuri zoezi la kuwatoa wafugaji katika maeneo ambayo hayakupangwa kwa shughuli za mifugo na kuwapeleka katika maeneo yaliyopangwa kwa kazi ya ufugaji.
“Sisi Wizara tumekusudia kufanya mapendekezo makubwa na tumeshakubaliana kuandaa na kupeleka mapendekezo kwa mamlaka za juu kuomba maeneo ambayo yatapangwa na kuwekewa miundombinu kama maji na majosho kwa ajili ya mifugo ili wafugaji waondoke katika maeneo ambayo yanawakutanisha na nyie wakulima,” alifafanua.
Pia Ulega aliwataka wafugaji hao kuanza kupanga mikakati ya kuvuna mifugo yao ili waanze kupata faida ya kipato na kusaidia kupunguza migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi.
“Hapa zitakuja milioni 200 za kutengeneza Mnada wa Chamgoi utakaowawezesha wafugaji wavune mifugo ili kunufaisha halmashauri, taifa na wafugaji wenyewe,” alibainisha.
Awali, wakulima wanaofanya shughuli zao katika wilaya hiyo akiwemo, Amiri Katundu wa Kijiji cha Dondo Dutani na Ramadhani Kingu wa Kijiji cha Kizapala kwa nyakati tofauti walisema wafugaji waliovamia wamewasababishia athari kubwa katika mashamba yao ikiwemo kukosa mavuno ya kutosha kwa sababu mifugo imekula mazao yao.
NA MWANDISHI WETU