WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amezionya halmashauri zinazokataa kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu.
Ummy amesema kitendo cha halmashauri hizo kugoma kutoa fedha katika makundi hayo, zinakiuka sheria ya fedha za serikali za mitaa na kanuni zake.
Waziri huyo alitoa onyo hilo mkoani Iringa, wakati akifungua kongamano la wanawake lililoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga, kusaidia kutangaza fursa kwa wanawake na kuwawezesha kiuchumi.
Ummy alisema kanuzi za sheria hiyo zinataka mikopo hiyo itolewe kwa vikundi vyenye sifa mbili ambazo ni kuanzisha biashara na vyenye biashara zinazohitaji kuendelezwa.
“Imezuka tabia katika halmashauri kukataa kutoa mikopo kwa vikundi vinavyotaka kuanzisha biashara vikiwemo vya wanawake mpaka viwe na biashara hai. Halmashauri zinatoa wapi utaratibu huu?”alisema huku akishangiliwa na wanawake hao.
Kwa vikundi vinavyotaka kuanzisha biashara, alisema halmashauri zinapaswa kujiridhisha kama maandiko ya biashara zao yanaweza kutengeneza mzunguko wa fedha wenye faida ya kuviendeleza na kufanya marejesho.
Alizitaka halmashauri hizo kuachana na ukiritimba na vikwazo vinavyoweza kuchangia kuchelewesha vikundi hususan wanawake kupata mikopo na kujiendeleza kiuchumi.
Pia alitoa onyo kwa baadhi ya vijana wanaonufaika na mikopo ya halmashauri hizo kutorejesha mikopo hiyo, hivyo serikali itaangalia uwezekano wa sehemu ya asilimia zinazotengwa kwao kuhamishiwa kwa wanawake.
“Katika asilimia 10 inayotolewa na halmashauri wanawake wanapata asilimia nne, vijana asilimia nne na walemavu asilimia mbili. Kuna shida ya urejeshaji wa mikopo inayotolewa kwa vijana na kama wataendelea hivyo, tutawanyang’anya asilimia mbili na kuihamishia kwa wanawake ili wawe na sita,” alisema.
Wakati huo huo, Ummy alisema mwaka 2021/2022 serikali kupitia asilimia 10 ya mikopo ya halmashauri inakusudia kutoa zaidi ya sh. bilioni 68.
Alisema kati ya fedha hizo zaidi ya sh. bilioni 27.6 zitanufaisha vikundi vya wanawake huku ikiangalia uwezekano wa kupunguza ukubwa wa wanachama wa vikundi kutoka watano hadi watatu.
Alitoa taarifa hiyo wakati akikabidhi mikopo ya zaidi ya sh. bilioni 1.1 kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu kutoka halmashauri zote tano za mkoa wa Iringa.
Awali, Sendiga aliwataka wanawake kutumia kongamano kuendeleza mahusiano na wasiwaone waliowatangulia kwa mafanikio kwamba wana majivuno.
Wakati huo huo, Ummy amewataka wakurugenzi wote nchini kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari kuzingatia muda wa wanafunzi wao kusoma na kufanya shughuli zingine za kifamilia.
Alisema kuna tabia ya watoto wanaosoma kwa muda mrefu ndio wenye uwezo wa kufaulu vizuri mitihani yao hatua inayofanya biashara ya elimu kwa njia ya mafunzo ya ziada kushamiri.
Waziri huyo alisema wizara yake inaendelea kuwasiliana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuchukua hatua madhubuti zaidi zitakazowanusuru vijana hao.
Na ESTA MALIBICHE, Iringa